SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

JULAI, 2017  James Kotei alikuwa anasaini mkataba mpya wa miaka miwili katika klabu yake ya Simba, hii ni baada ya utendaji wake kuwaridhisha mabosi wake, hiyo akiwa ameitumikia kwa miezi sita tu.

 Mkataba huo ulifikia tamati mwishoni mwa msimu huu, sasa  kuna kitendawili ndani ya Simba, kama atabaki au atafunguliwa mlango wakwa heri.

Pacha wake eneo la kiungo, Jonas Mkude ambaye mkataba pia ulifikia tamati, tayari ameishasaini mwingine mpya wa miaka miwili, wakati huo  Kotei akiendelea kujifua ufukweni kwao Accra, Ghana akisikilizia simu kutoka kwa viongozi.

Kuna kundi linadai  Mghana huyo hayupo kwenye mahitaji ya Mbelegiji, Patick Aussems habari hizi unaweza kuzipata kwa undani sana kufikia wachokozi wa mambo masuala ya soka la Bongo.

Uwezo wa Kotei na mahitaji ya Simba yanaweza kukufanya ukakumbuka filamu ya Amis Tambwe mfungaji bora wa  Ligi Kuu Tanzania Bara 2014 (mabao 19), aliyetupiwa virago na kocha, Patrick Phiri na kukaribishwa sofa na klabu ya Yanga.

Alichokifnya Tambwe msimu wake wa kwanza tu  Yanga  ni kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni  kufunga mabao mengi zaidi (21), ikiwa ni chachu ya timu  kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Terejee kwa Kotei, kiungo bora wa msimu ndani ya klabu yake ,  tuzo za MO Simba 2019 Award akiwapiku  Mzamiru  Yassin na Jonas Mkude waliokuwa katika kinyanganyiro  hicho.

Mbali na kukamilisha majukumu yake eneo la kiungo, lakini pia  ndiye  aliyekuwa akitumika kama kiraka, akicheza beki wa kulia pamoja na beki wa kati kwa nyakati tofauti.  Unaweza usema ni Erasto Nyoni mwingine ndani ya Simba.

Kotei  mwenye urefu wa futi tano hana mambo mengi uwanjani, hana darizi, hana  matobo, wala humuoni akikokota mpira umbali kadhaa, lakini  jukumu lake mama ni kuwalinda mabeki wake, kukaba  mtu na majukumu yake amekuwa akiyafanya vema kwa kipindi chote tangu alipotua Msimbazi.

Katika maisha yake ya soka la ushindani Simba ni timu yake ya pili kuichezea mechi nyingi (60) tena kwa mafanikio akiwa kwenye ubora mkubwa mbali na Liberty Professionals ya kwako Ghana.

Maneno  kiduchu tu yaliyotoka kinywani mwa Mwenyekiti wa Kamati ya  usajili Simba, Zachari Hans Pope kwamba wanamletea Mkude mwaume mwingine eneo la kiungo  wakati huo hadi leo  maneno hayo yanaishi. Kotei kadhihirisha  hilo.

Ikitokea Kotei ameondoka kweli Simba atakuwa ni Patrick Mutesa Mafisango  mwingine. Tofauti ikiwa ni aina ya kuondoka tu. Ni bora ulichonacho  kimepitia milima mingi  na mabonde unakiongezea vitu vichache tu katika maboresho kuliko kutarajia makubwa kwa kipya uletachao.

Kwa nini Sharif Eldin  kutoka Sudan asaini mwaka mmoja? Kuna uoga. Tangu  2016 alipojiunga na  Al Hilali mafanikio makubwa ya klabu hiyo kwenye  Ligi ya Mabingwa ni  kufika  hatua ya 16 bora pekee (2017).

Mwaka jana hao hao Al Hila ya Eldin iliishia hatua za awali tu. Maana yake Kotei alicheza mechi nyingi  zikiwamo  dhidi ya timu kubwa, Al Ahly, TP Mazembe, AS Vita, JS Saoura kuliko ingizo hilo jipya. Mapungufu yake yapo wapi?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here