SHARE

NA MWANDISHI WETU

BILA kuwa na Simba madhubuti, hakuna Yanga imara, ukisema hivi wenyewe wanajua.

Ndiyo asili ya ukaribu wa klabu hizi kongwe zenye mtaji mkubwa wa rasimali watu.

Neno hili limekuwa likirudiwa tangu zama za viongozi wa zamani, akina Amir Bamchawi, Simba, kadhalika enzi za Mwenyekiti wa Yanga, Mangala Tabu.

Nilichukua muda mrefu kulielewa, pengine kama siyo kipindi kile alichojiweka pembeni Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji basi hadi hii leo kwangu ungekuwa msamiati mgeni.

Lakini sasa hata ukiniamsha saa tisa usiku nikiwa na usingizi wa pono, ukiniuliza maana ya Simba madhubuti huzaa Yanga imara nitakwambia.

Kwamba, hawa ni watoto mapacha pengine nitumie usemi huu, alichokifanya mmoja na mwingine atapenda kukitenda, japo kiwe kibaya au kizuri.

Mmoja akishika kaa la moto na mwingine atashika pia, hili la kuungua litajulikana baadaye.

Msimu uliopita tulishuhudia kebehi zilizoelekezwa Yanga, hususan katika zoezi lao lile la kuchangisha fedha za masurufu ya wachezaji, katika mechi zao mbalimbali za Ligi.

Walifanya hivyo ili kupunguza makali ya ukata, kutokana na timu hiyo kutokuwa na mfadhili.

Waliocheka walimaliza kila staili na waliosifu pia walikuwepo, pongezi zilimwendelea kocha aliyeipitisha Yanga katika kipindi hicho kigumu, Mwinyi Zahera.

Raia huyo wa DRC alisifiwa kwa kuleta umoja wa Wanayanga, na mshiamano kwa wachezaji. Ndani ya kikosi chake mchezaji aliyefikia uamuzi wa kugoma ni kipa tu, Beno Kakolanya.

Wengine walikubali yaishe hadi wakamaliza ligi wakiifikisha timu yao karibu ya kilele, nafasi ya pili kati ya timu 20 si haba.

Sasa yale yaliyotokea kwa Yanga, ‘pacha’ wake naye anatamani, ana hamu naye afanye kama ilivyokuwa kwa wenzake, kama shida au faraja itajulikana hapo mbele.

Kimgogoro hichooo kinanukia, na kama leo hakipo leo basi kesho kinakuja maana wanaotuhumiana hawajatoka hadharani na kukanusha wakipeana mikono, ilihali wanaweza kufanya hivyo.

Hawajajitokeza wakasema “Tunasingiziwa hatuna mgogoro” na pengine tukaona picha wakikumbatiana kama zile wanazotoa saa saba, kuna ugumu gani?.

Kama tunaona picha za mchezaji aliyepanda ndege zikipigwa kwa bashasha na viongozi wakionyesha alama ya vema kwa vidole vyao, kwa nini hawa wanaodai hakuna mkwaruzano wasitupie picha za kudhihirisha umoja na upendo wao?

Dawa nyingi huwa chungu, lakini ndiyo zinazoponya na hili kwa Wanasimba ni heri wakatambua kwamba ndani ya klabu yao ipo Sintofahamu, na kama haipoi basi iko njiani.

Kwa matukio kama haya, ndiyo unapoweza kupata tafisiri pana niliyoirudia mara kadha pale juu, kwamba Bila Simba madhubuti basi hakuna Yanga Imara!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here