SHARE

NA AYOUB HINJO


MICHEZO ya kutafuta nafasi ya kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani huko nchini Cameroon iliendelea hivi karibuni kwa timu mbalimbali kucheza katika makundi yao.

Kila timu ilifanikiwa kucheza mchezo wa pili kwa kila kundi baada ya ile ya kwanza kupigwa mwaka jana sehemu tofauti barani Afrika.

Kubwa zaidi ni maendeleo ya timu kutoka katika ukanda wa Afrika Mashariki ambazo zinatafuta nafasi hiyo baada ya Uganda kufanikiwa kufanya hivyo mwaka juzi nchini Gabon.

Je, kwa aina ya matokeo ambayo wanapata timu za ukanda wa Cecafa, kuna matumaini yoyote kwa wao kupata nafasi ya kusonga mbele?

Hakika hilo ni swali ambalo kila mmoja wetu kutoka Afrika Mashariki atakuwa anajiuliza, ni furaha ya kila mtu kuona timu hizo zinafanya vizuri na kutanua wigo wa soka la ukanda huu wa Cecafa.

Mpaka sasa tunawakilishwa na timu tano ambazo ni Tanzania na Uganda waliopo Kundi L, Kenya wapo Kundi F, Burundi nao kwenye Kundi C na Rwanda wametupwa katika Kundi H.

Ndoto za kila mmoja ni kuona timu zote hizo zinasonga mbele na kutinga katika michuano hiyo mikubwa ndani ya Bara la Afrika.

Itawezekana? Kama Uganda ilifanikiwa kwenda Gabon mwaka juzi hata kwa wengine nafasi ipo kama watafanya vizuri katika michezo yao iliyobaki.

TANZANIA NA UGANDA

Wakati makundi yamepangwa, timu za Tanzania na Uganda kwa pamoja ziliunda Kundi L sambamba na Lesotho na Cape Verde.

Baada ya michezo miwili Uganda wapo nafasi ya kwanza, wakiwa na pointi nne, wakifuatiwa na Lesotho pointi mbili, sawa na Tanzania wakitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na Cape Verde inashika mkia ikiwa na pointi moja.

Michezo minne imebaki kwa kila timu, ina maana kuwa kundi lao bado liko wazi kwa yeyote kufanya vizuri na kusonga mbele kwa kutoa timu mbili tu.

Juni 10, 2017, mchezo wa kwanza Tanzania walicheza dhidi ya Lesotho katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na kufanikiwa kutoa sare ya kufungana bao 1-1.

Straika tegemeo wa kikosi cha Tanzania, Mbwana Samatta, alifanikiwa kufunga bao dakika ya 28 kwa mkwaju wa faulo, kabla ya mshambuliaji wa Lesotho, Thapelo Tale kusawazisha dakika ya 35 baada ya kuwashinda ujanja mabeki wa timu pinzani.

Upande wa pili Uganda walifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Cape Verde, huku straika Geoffrey Sserunkuma akitumia nafasi hiyo baada ya mabeki wa wenyeji wao kufanya makosa.

Mchezo wa pili wa Taifa Stars ulipigwa Septemba 8 katika Uwanja wa Mandela dhidi ya wenyeji wao, Uganda, ambao ulimalizika kwa suluhu huku mashabiki wa Tanzania wakionekana kufurahishwa na kiwango cha timu hiyo.

Hata mchezo mwingine wa kundi hilo uliozikutanisha Lesotho na Cape Verde ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 na kufanya kundi hilo kushindwa kutoa mwelekeo.

Oktoba 10 mwaka huu, michezo ya kutafuta tiketi kushiriki michuano ya Afrika Mashariki itaendelea, huku Tanzania akitarajiwa kusafiri hadi Cape Verde na Lesotho akiwa mwenyeji wa Uganda kabla ya kuwa na marudiano siku tatu baadaye kwa timu zote.

RWANDA

Katika michezo miwili waliyofanikiwa kucheza mpaka sasa, hawajafanikiwa kupata ushindi wowote kwenye Kundi H, ambalo lina timu za Ivory Coast, Guinea na Afrika ya Kati.

Vijana hao wa Paul Kagame, Juni 11 walifungwa mabao 2-1 mchezo wa kwanza  waliocheza dhidi ya Afrika ya Kati katika Uwanja wa Barthelemy Boganda uliopo kwenye Mji wa Bangui.

Kisha wakapoteza mchezo wa pili kwa mabao 2-1 dhidi ya Ivory Coast uliopigwa katika Uwanja wa Nyamirambo, Kigali na kuwafanya kushindwa kuwa na pointi mpaka sasa.

Mchezo wa tatu ambao utapigwa Oktoba 10 watacheza dhidi ya Guinea katika Uwanja wa Septemba 28, huku wenyeji hao wakiwa ni vinara wa kundi hilo baada ya kushinda michezo yote miwili dhidi ya Ivory Coast na Afrika ya Kati.

Rwanda wamebaki na michezo minne ambayo itawafanya kuhitaji ushindi wa lazima ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele, ikiwa mpaka sasa hawana pointi yoyote.

KENYA

Timu nyingine ya ukanda wa Cecafa ambayo ipo katika Kundi F linaloundwa na Ghana, Sierra Leone na Ethiopia, wote wana pointi tatu baada ya kucheza michezo miwili.

Mchezo wa kwanza Kenya walichezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Sierra Leone katika Uwanja wa Taifa uliopo ndani ya Mji wa Freetown.

Lakini mchezo wa pili timu hiyo kutoka Afrika Mashariki walimwezesha Rais, Uhuru Kenyatta, kutabasamu baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ghana katika Uwanja wa Moi International Sports Center ndani ya Mji wa Kasarani.

Mchezo wa kukamilisha hatua ya kwanza katika kundi hilo wanatarajia kuchezwa dhidi ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Bahir Dar nchini humo.

Bado Kundi F hakuna aliyejihakikishia nafasi ya kusonga mbele, ikiwa timu zote nne zilizopo zimefanikiwa kupata pointi tatu kwa kushinda mchezo mmoja na kufungwa mmoja.

Kenya bado nafasi wanayo kama watafanikiwa kushinda michezo yao yote iliyobaki.

BURUNDI

Mapema kabisa wakati ratiba inatoka, Burundi walipangwa katika Kundi C lililo na timu za Mali, Gabon na Sudan Kusini.

Baada ya kuchezwa michezo miwili mpaka sasa, Burundi wamefanikiwa kupata pointi nne wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Mali, wenye pointi sita kwa kushinda michezo yote miwili.

Burundi walianza kampeni hiyo kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sudan Kusini katika Uwanja wa Prince Louis Rwagasore uliopo mjini Bujumbura.

Kisha walisafiri mpaka nchini Gabon katika Uwanja wa d’Angondje na kutoa sare ya kufungana bao 1-1, wakifanikiwa kurudi kwao na pointi moja pekee iliyowawezesha kukaa nafasi ya pili.

Katika michezo minne iliyobaki wataanza kwa kucheza na timu ya Taifa ya Mali huko kwenye Uwanja wa Mars 26, uliopo ndani ya Mji wa Bamako.

Kwa kasi waliyoanza nayo wanaonyesha uhai mkubwa na ahueni, huku kila mmoja kutoka Afrika Mashariki akitamani kuiona timu hiyo ikisonga mbele kutafuta safari ya kuingia Cameroon kwa nguvu.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here