Home Makala JAMES RODRIGUEZ NI MTAMU SANA ILA HAWEZI KUFANYA KAZI NA MOURINHO

JAMES RODRIGUEZ NI MTAMU SANA ILA HAWEZI KUFANYA KAZI NA MOURINHO

403
0
SHARE

MANCHESTER, England

JINA la James Rodriguez si geni kwa wapenzi wa soka. Kila mmoja anafahamu ubora wake anapokuwa na mpira mguuni.

Lakini kwa sasa habari kubwa inayotikisa kutoka kwake si mabao yake, ishu ni juu ya uhamisho wake.

Ndiyo, Real wako tayari kumuuza fundi huyu wa mpira aliyebeba kiatu cha ufungaji bora wa Kombe la Dunia mwaka 2014, kule Brazil na tetesi zinaonyesha James anaelekea kutua Old Trafford, kujiunga na Manchester United.

Kwa nini James anaondoka Madrid? Je, Man United ni sehemu sahihi kwake? Haya ndiyo maswali mawili makubwa ambayo mashabiki wa soka wamekuwa wakijiuliza hivi sasa.

Kama tunakumbuka James alisajiliwa na Madrid akitokea Monaco, Julai 2014, baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia.

Na alianza maisha yake Bernabeu kwa kasi ya ajabu. Kila alipopewa nafasi, hakufanya makosa. Alicheza kwa bidii na kuonyesha kuwa ilikuwa ndoto zake kuvaa jezi ya Real Madrid.

Kipindi cha nyuma kidogo, Aprili 2014, akiwa bado mchezaji wa Monaco, James aliwahi kupanda ndege hadi Ujerumani kuushuhudia mchezo wa nusu fainali Ligi ya Mabingwa, Real wakicheza na Bayern Munich.

Ungemwambia nini James kuhusu Madrid? Ni klabu aliyoipenda kutoka ndani ya moyo wake.

Haikuwa shida sana kwa wakala Jorge Mendes kukaa mezani na Rais wa Madrid, Florentino Perez kukamilisha dili hili la James.

Chini ya Carlo Ancelotti, James alitumika kama kiungo mshambaliaji na wakati mwingine kama winga wa pembeni na kuiongoza Real kubeba mataji mawili, UEFA Super Cup na Klabu Bingwa ya dunia.

Rodriguez alimaliza msimu kwa kufunga mabao 17 na kutoa asisti 15, na kufanya Wachambuzi wengi wa soka nchini Hispania kumtabiria makubwa ndani ya Bernabeu.

Lakini mambo yalibadilika mwaka 2015, Rafa Benitez alipoteuliwa kuwa kocha mpya wa Madrid. Ugomvi ulianza mwanzoni mwa msimu, Rodriguez alipochelewa kujiunga na timu akitokea kwao Colombia.

Tatizo likazidi tena baadaye, pale James alipolazimisha kucheza mechi ya Taifa lake na kuumia msuli, jeraha lililomuweka nje kwa miezi zaidi ya mitatu.

Benitez hakuweza kuvumilia zaidi, akatoka hadharani na kusema kuwa James ameporomoka kiwango kwa kuendekeza starehe na kuchukia mazoezi, hivyo mwili wake kuongezeka kwa kilo kadhaa.

Benitez alisusa kumpanga James kwenye mechi kadhaa na baadaye nyota huyo alijiunga na timu yake ya Taifa na kufunga bao dhidi ya Chile, kisha kutoa ujumbe kuwa yuko vizuri kuliko watu wanavyomfikiria.

“Bao hili ni salamu kwa waliokuwa wakisema nimenenepa na siko kwenye kiwango bora,” alisema James baada ya mchezo huo.

Stori za Rodriguez kuzurura usiku kwenye klabu kubwa za Madrid, zilitikisa vyombo vya habari vya Hispania, ambapo mwandishi Ivan Mejia, alinukuliwa akisema, “Amepoteza heshima yake. Kama hatatulia na kujirekebisha huu unaweza kuwa mwisho wake.”

Lakini mwisho wa siku James ndiye aliyeibuka mshindi katika bifu hili baina yake na Benitez, kwani baadaye bosi wa Madrid, Perez alichukua uamuzi wa kumsimamisha kazi kocha huyo.

Zinedine Zidane akapewa kazi na baadaye ikagundulika kuwa tatizo halikuwa Benitez, baada ya James kuendelea kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza cha Madrid.

Zidane alianza kazi kwa kumuamini James, lakini muda kidogo, kiungo mwingine wa Hispania, Isco aliibuka na kuonyesha kiwango bora kilichomfanya apewe nafasi mbele ya Mcolombia huyu.

Isco alionekana kuwa mpambanaji na yupo tayari kujitoa kwa Madrid kuliko alivyokuwa James, hapa kazi ikawa rahisi kwa Zidane kwenye kufanya uchaguzi wa kikosi cha kwanza. James akatupwa benchi!

Ndoto za James kutaka kupata mafanikio akiwa na Real zimekufa na sasa anawaza kitu kimoja tu kwenye kichwa chake, siku atakayoondoka Santiago Bernabeu.

Kuibuka kwa kina Marcos Asensio na Lucas Vazquez, ni tishio zaidi kwa James. Vijana hawa wana kasi, nguvu na ni wapambanaji pale timu inapokuwa haina mpira, ni ngumu kwa Rodriguez kuendelea kutamani kubaki Madrid.

“Mimi ningemshauri atafute timu atakayopata nafasi kwenye kikosi cha kwanza na si kukubali kuendelea kukaa benchi Real Madrid,” alinukuliwa mjomba wake James, Juan Carlos Restrepo alipokuwa akifanya mahojiano na kituo kimoja cha redio nchini Hispania.

Rodriguez ni mchezaji wa hadhi ya dunia, ana kipaji kikubwa na anaweza kurudi kwenye ubora wake akijiunga na timu kubwa kama Manchester United Chelsea.

James anaweza kutua Premier League, vigogo wa England hawatakuwa na shida yoyote ya kutumia kiasi cha pauni Mil 60 kwa ajili ya kuinasa saini ya fundi huyu wa mpira.

Lakini kwa kumtazama Jose Mourinho  ni wazi kuwa chaguo sahihi kwa James ni kwenda Chelsea na si Manchester United.

Mchezaji aliyekuwa kwenye kichwa cha Mourinho kwa wakati huu ni straika wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann, si James.

Jose hawezi kuishi na wachezaji wajivuni, wenye mdomo mwepesi wa kuongea na vyomo vya habari kuhusu hali ya timu.

Ni ngumu kwa Mourinho kukubali kufanya kazi na wachezaji wenye kuchagua muda gani anataka kufanya mazoezi au kujiunga na timu, tabia za James ni tofauti kabisa na wachezaji ambao Jose angependa kufanya nao kazi kwa sasa.

Kwa sasa James anatakiwa kupata timu itakayompa nafasi na kumuamini ili aweze kurudi kwenye ubora wake, lakini kwa tabia zake ni ngumu sana kupata matunzo hayo chini ya Jose Mourinho.

Takwimu za James Rodriguez msimu huu:

Mechi alizocheza 30

Alizoanza 13

Mabao 11

Assisti 8

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here