Home Michezo kitaifa JAY MSANGI NGUMI ZA KULIPWA ZIMEPOTEZA MVUTO

JAY MSANGI NGUMI ZA KULIPWA ZIMEPOTEZA MVUTO

473
0
SHARE

NA MARTIN MAZUGWA,

KARIBU msomaji wa safu hii ya ITS SHOW TIME, ambayo inakujia kila Jumatano ambapo unapata fursa ya kujua mambo mengi kuhusiana na mchezo wa ngumi pamoja na mabondia.

Mchezo huu ambao kila siku umekuwa ukipanda chati kwa kasi ulimwenguni,  huku nchini Tanzania hali ikizidi kuwa mbaya kutokana na usimamizi mbovu pamoja na migogoro isiyokwisha katika vyama vinavyousimamia mchezo huo.

DIMBA lilipata nafasi ya kufanya mazungumzo na mmoja kati ya mapromota anayefanya vizuri hapa nchini kwa kuandaa mapambano makubwa, Jay Msangi, ambaye amefunguka mambo mengi ikiwemo sababu zinazopelekea mchezo wa ngumi kuporomoka kwa kasi hapa nchini miaka ya hivi karibuni  tofauti na miaka ya nyuma.

Unadhani nini kinasababisha anguko la mchezo wa ngumi hapa nchini?

Hakuna umoja tena baina ya viongozi wa vyama vya ngumi za  kulipwa hapa nchini ambao wamekuwa wakilumbana kila kukicha, jambo linalopelekea mabondia kuyumba.

Nini kinakwamisha maendeleo ya ngumi za kulipwa hapa nchini?

Yapo mengi yanayokwamisha maendeleo ya ngumi za kulipwa, kubwa ni urasimu wa viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza mchezo huu, kitu kinachosababisha twende hatua tatu mbele na kurudi hatua tano nyuma, jambo ambalo linatia aibu.

Unafikiri nini sababu inayopelekea mabondia wengi kupoteza mapambano nje ya nchi?

Mabondia wengi hapa nchini wamekuwa na kawaida ya kukamiana wanapocheza mapambano ya ndani ya nchi ili kuwekeana heshima na kuondoa ubishani kwa mashabiki wao kuhusu nani ni bora  miongoni mwao, ndio maana unakuta kunakuwa na mchuano mkali, tofauti na wanapotoka kwenda kucheza nje ya nchi ambapo wamekuwa wakipoteza kirahisi kwani  wanakuwa wanaangalia zaidi fedha kuliko heshima.

Pambano gani lilikupa wakati mgumu zaidi kuliandaa tangu ulipoanza kuandaa mapambano hapa nchini?

Kati ya mapambano yaliyowahi kunitesa kiasi cha kufikiria kupumzika kuandaa mapambano, ni kati ya Abdalah Pazi ‘Dulla mbabe’ dhidi ya Chengbo Zeng, lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, lilinisumbua sana kwani nilitumia gharama kubwa kuliandaa na lilikuwa likipigwa vita sana.

Unafikiri Waziri Nape Nnauye afanye nini kunusuru ngumi za kulipwa? 

Namuomba Waziri Nape aangalie kwa makini suala la migogoro ya mara kwa mara katika mchezo wa ngumi, kwani unakoelea si kuzuri, hakuna tena umoja baina ya vyama vinavyousimamia mchezo huu hapa nchini, kitu kinachopelekea mchezo huu kushuka thamani hapa nchini.

Mara baada ya kuandaa pambano la Cheka na Vijendar Singh nchini India, kuna pambano jingine unatarajia kuandaa siku za karibuni?

Ndio baada ya Francis Cheka kupigwa kwa mizengwe nchini India, kuna pambano la kihistoria linakuja baina ya familia  mbili;  kati  ya Cheka dhidi ya singh  ambapo mdogo wa  Vijendar, atapanda ulingoni dhidi Cosmas, wakati Francis atakapohitaji kulipa kisasi siku hiyo.

Pambano hilo linatarajiwa kupigwa nchini Tanzania ikiwa ni nafasi ya Francis Cheka kulipa kisasi dhidi ya Vijendar.

Sheria ya mchezo wa ngumi  inasemaje kuhusu malipo ya  bondia, anapaswa kulipwa kabla ya pambano au baada kupanda ulingoni?

Hii ipo zaidi nchini Tanzania ambapo mabondia wamekuwa wakitaka kulipwa stahiki zao kabla ya kupanda ulingoni, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za mchezo wa ngumi ambapo bondia anatakiwa kulipwa mara baada ya kupanda ulingoni.

Nje ya upromota, wewe ni mtu wa aina gani na unajishughulisha na nini?

Ukiachana na upromota, mimi ni mjasiriamali ninajishughulisha na ufugaji wa ng’ombe na kuku, muda wangu wa mapumziko huwa nautumia katika miradi hiyo.

Nini wito wako kwa mabondia wanaocheza ngumi za kulipwa hapa nchini?

Wito wangu kwa mabondia wa hapa hasa wanaocheza ngumi za kulipwa, wanapaswa kuwa makini na afya zao kabla ya kupanda ulingoni wahakikishe wanapima afya zao.

“Niliwahi kushuhudia mabondia sita wakishindwa kupanda ulingoni kutokana na kushindwa kufaulu vipimo vya afya kutokana na kukutwa na magonjwa ya kuambukiza kama PSB na HIV, lakini nikawakuta wanacheza mapambano ya mtaani,” alisema.

Pia naomba mabondia waache kuyumbishwa na mapromota uchwara ambao wamekuwa wakiwatumia na kuwaacha bila kuwapa msaada wanapopata matatizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here