SHARE

LAS VEGAS, Marekani


KABLA ya kupanda ulingoni kupambana na Conor McGregor, Floyd ‘Money’ Mayweather, alitangaza hadharani kuwa hatapigana tena baada ya pambano hilo kumalizika.

Siku ikafika na dunia ikamshuhudia Mayweather akipanda ulingoni kumshikisha adabu mbishi McGregor kwa ‘TKO’, katika raundi ya 10, akiweka rekodi ya kucheza mapambano 50 bila kupigwa.

Kama ilivyokuwa kwa Marcos Maidana na Manny Pacquiao, pambano hili pia lilimalizika kwa mashabiki kuendelea kunung’unika, japo awamu hii maneno yalikuwa tofauti kidogo.

Katika mapambano hayo mawili, mashabiki wa masumbwi duniani walimshutumu Mayweather kwa kupata ushindi wa kubebwa na majaji, lakini dhidi ya McGregor, malalamika yamekuja kivingine.

Safari hii wadau wamelalamika juu ya mambo mawili. Kwanza ni ubora wa McGregor, na pili ni kuwapo kwa dalili za mpambano huu kupangwa ili Mayweather apige hela na kuweka rekodi ya kutopigwa kwenye mapambano 50.

Tuanze na ubora. Huu ulikuwa mpambano wa kwanza kwa McGregor kucheza kama mwanamasumbwi kamili ‘boxer’. Imekuwaje akapata vigezo vya kupambana na Mayweather, bingwa asiyepigika?

McGregor ni bingwa wa michezo ya mateke na ngumi, maarufu kama ‘MMA’, hivyo ilimhitaji muda zaidi ya kujifunza ngumi tupu, ili aweze kucheza na Mayweather.

Baadhi pia walihoji kwanini McGregor hakupata mapambano yoyote ya ngumi kwanza ili kujipima ubora wake kabla ya kupigana na Maywether. Tuseme alikuwa hatambui ubora wake?

Maswali haya ndiyo yakaleta watu kwenye hoja ya pili kuwa wawili hawa walipanga huu mpambano ili kutengeneza pesa chafu na rekodi nzuri kwa Mayweather.

Kinachoaminiwa ni kuwa, kama Mayweather alikuwa na nia kweli ya kusaka rekodi hiyo, angeweza kukubali pambano la marudiano na Manny Pacquiao au kucheza na Amir Khan, kwanini alimchagua MacGregor?

Dhana hizi ndio zimefanya hata wadau wengi wa mchezo wa ngumi kutokubaliana na maneno ya Mayweather kuwa hatapigana tena baada ya pambano lile la McGregor. Kwanini?

Hii si mara ya kwanza kutangaza kustaafu, aliwahi kufanya hivyo kabla. Awali alitangaza kustaafu baada ya kumchapa Andre Berto, mwaka 2015, lakini miaka miwili alibadili msimamo wake na kucheza dhidi ya McGregor.

“Nimeshatoa msimamo wangu na hili sirudi nyuma tena,” alisema Mayweather, baada ya kumalizika kwa pambano lake dhidi ya Berto.

“Safari hii ni tofauti kidogo. Hili nimeshirikisha watoto wangu na sijawahi kuwadanganya. Mwisho umefika sasa na ninashukuru kwa nyakati zote.

“Huu ulikuwa mchezo bora kwangu. Nimemaliza safari yangu kwa pambano bora mno.”

Maneno haya haya ameyarudia tena baada ya kumalizika kwa pambano lake dhidi ya McGregor. “Hili ni pambano langu la mwisho. Hakika, sitapigana tena. Nimechagua bondia bora wa kupigana naye na nikushukuru Conor kwa wakati wako,” alisema Mayweather.

Japo McGregor anaweza kuomba mpambano wa marudiano, lakini hili linaweza kuwa gumu kidogo. Conor ni mpiganaji wa MMA, na kuna kila dalili za kurudi kwenye mchezo wake huo na kama akiamua kurudi tena ulingoni, basi mpinzani atakayemchagua ni Paulie Malignaggi.

Vipi kwa Mayweather, huu ni mwisho kweli? Katika hili, bondia huyu mwenye miaka 40, alikuwa na jibu hili: “Sifikirii kurudi tena ulingoni kwa sasa, ni wakati wa kutulia na familia yangu na kutafuta warithi wangu kwenye fani hii.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here