SHARE

ALIYEKUWA Nahodha wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’, alitangaza kustaafu kucheza soka hivi karibuni, ambapo mwishoni mwa wiki hii mchezaji huyo aliagwa rasmi katika kikosi cha timu hiyo.

Mgosi ambaye aliitumikia Simba kwa takribani misimu 10 kwa nyakati tofauti, aliagwa Jumapili wakati timu yake ilipocheza mechi ya kirafiki dhidi ya URA ya Uganda, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mgosi aliagwa kwa heshima kwa kuichezea timu yake dakika tano kabla ya kuvua kitambaa cha unahodha na kumkabidhi Jonas Mkude huku yeye akibaki kuwa kama meneja wa timu hiyo.

Je, ukiwa kama mdau wa soka Tanzania unazungumziaje suala la mchezaji huyo kuamua kustaafu soka kwa kipindi hiki?

Unaweza kutoa maoni yako kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno ukianzia na jina lako na mahala ulipo.

 

MAJIBU YA WIKI ILIYOPITA

Mada ya wiki iliyopita ilikuwa ikizungumzia juu ya usajili wa Simba, kutokana na jinsi kikosi chake kilivyo je, wamefanya usajili mzuri ukilinganisha na misimu iliyopita?

Wachangiaji wengi walielezea juu ya usajili huo ambao asilimia kubwa ya wachangiaji walikubali kuwa usajili huo ni mzuri na pengine unaweza kutisha msimu ujao.

Utata huo ulikuja kutokana na klabu hiyo kushindwa kufanya vizuri kwa takribani misimu mitatu sasa, na hilo ni kutokana na usajili unaoitwa wa bei rahisi waliokuwa wanafanya viongozi wa timu hiyo.

Lakini sasa Simba imekabidhiwa fungu la usajili kutoka kwa mwanachama wa timu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, ambapo fedha hizo zitatumia kusajili wachezaji wazuri.

Naitwa Elia Sanare wa Kurasini, Simba imesajili vizuri lakini Yanga ina kikosi kizuri na imewaongeza nyota wazuri na itaendelea kutesa Ligi Kuu Bara.

 

*****

Jina langu ni Victor Loth wa Singida, inawezekana Simba ikiwa nzuri na Mavugo anaweza kumpiku Ngoma, maana kuna Kichuya, Ajibu na Lyanga wataunda kombinesheni nzuri.

 

*****

Naitwa Festo Kaduma wa Iringa, Simba mwaka huu ni kwetu, usajili uliofanywa pamoja na benchi la ufundi lipo vizuri, tusubiri ligi ianze tuwaonyeshe.

 

*****

Mimi ni Athuman Majeshi wa Tanga, usajili uliofanywa na Simba si wa kutisha sana, kinachotakiwa ni viongozi kuwa na mshikamano na wajipange kutwaa ubingwa si kuweka heshima kwa kuifunga Yanga tu.

 

*****

Naitwa Kunibeti Chikawe wa Lindi, nina imani usajili wa safari hii utaisimamisha Yanga kutokana na viongozi kutoingilia usajili wa kocha na Mavugo ni kama Okwi, hivyo atasumbua sana akipewa ushirikiano na wenzake.

 

*****

Naitwa Makene Adam wa Mwanza, ukilinganisha utaona Simba bado haijakaa vizuri, ndio wanajenga timu na bado hawaezi kama timu, wenzao wamekaa muda mrefu na wamecheza mechi nyingi na kuzoeana sana.

 

****

Naitwa Penford Ainea wa Dar es Salaam, Simba ya msimu huu iko vizuri ukilinganisha na misimu iliyopita kwa kila safu kwani tutarajie kombinesheni nzuri ya Ajibu, Mavugo na Kichuya.

 

*****

Jina langu ni MR Mtepe wa Magomeni, safari ya ligi ni ndefu sana na huwezi kuipima timu kwa mchezo mmoja wa majaribio waliocheza hasa kwa timu dhaifu kama AFC Leopards, macho yangu kwa Simba hadi icheze angalau mechi 10 na kuangalia matokeo yao ndio unaweza kujadili usajili wao.

 

*****

Naitwa Chageni wa Arusha, usajili wa Simba ni kwa ajili ya ligi na si Yanga, Mavugo anahitaji muda ili kuielewa vizuri Ligi ya Tanzania.

 

*****

Naitwa Hassan Mdoe wa Malalao Mwangoi, usajili wa Simba mwaka huu ni mzuri, Yanga wajiandae.

 

****

Naitwa Abdul Makambo wa Msasani, usajili wa Simba ni mzuri, Simba kila mwaka ina kawaida ya kufanya usajili wa wachezaji wenye viwango vya hali ya juu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here