Home Michezo Kimataifa Jean Tigana: Mfaransa aliyefananishwa na Ally Yusuf

Jean Tigana: Mfaransa aliyefananishwa na Ally Yusuf

421
0
SHARE

NA HENRY PAUL

JINA la kiungo mshambuliaji nyota wa Ufaransa, Jean Tigana, si geni masikioni mwa wapenzi wa soka ulimwenguni kote, kwa sababu ni miongoni mwa wachezaji wachache wanaokumbukwa kutokana na uhodari wao wa kumudu kucheza vyema nafasi ya kiungo mshambuliaji.

Pamoja na uwezo huo mkubwa aliokuwa nao pia nyota huyo wakati wa enzi zake za kucheza soka ya ushindani alikuwa akionesha vitu adimu uwanjani ikiwa ni pamoja na kupiga chenga, kutoa pasi na uwezo mkubwa wa kupachika mabao.

Kutokana na umahiri wake mkubwa awapo uwanjani, wapenzi wa soka ulimwenguni hususan wa Ufaransa walimchukulia mchezaji huyo kama ni mmoja wa kiungo bora wa miaka ya 1980.

Tigana wakati wa enzi zake za kucheza soka ya ushindani kwa kipindi cha miaka 17 kuanzia mwaka 1975 hadi 1991, amezichezea timu kadhaa kwa mafanikio ikiwemo Toulon, Lyon, Bordeaux na Marseille zote za Ufaransa.

Akiwa na klabu ya Bordeaux misimu mitatu kuanzia 1983/1984 hadi 1986/1987, Tigana alikuwa ni mmoja wa wachezaji walioiwezesha klabu hiyo kutwaa taji la Ligi Daraja la Kwanza Ufaransa maarufu kama French Division 1 na taji la Coupe de France, misimu miwili 1985/1986, 1986/1987.

Pia akiwa na Olympique de Marseille misimu miwili 1989/1990, 1990/1991 Tigana alikuwa ni mmoja wa wachezaji wa klabu hiyo walioiwezesha kutwaa taji la Ligi Daraja la Kwanza Ufaransa ambapo wakati huo kiungo huyo alikuwa na kiwango cha juu.

Tigana pamoja na kuzichezea timu hizo kwa mafanikio, pia ameichezea timu ya Taifa ya Ufaransa kwa kipindi cha miaka tisa kuanzia 1980 hadi 1988 ambapo katika kipindi hicho aliweza kuichezea mechi 52 na kuifungia bao moja.

Pia kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kumudu kucheza vyema nafasi ya kiungo mshambuliaji, mwaka 1984 alichaguliwa mchezaji bora wa Ufaransa na alitwaa tuzo ya mshindi wa pili Ballon d’ Or, Onze d’Argent na Onze de Bronze 1987.

Ufundi na uwezo mkubwa aliokuwa nao nyota huyo wa kumudu kucheza vizuri dimba la kati, wapenzi wa klabu ya Manyema msimu wa 1991/1992 waliufananisha na kiungo mshambuliaji wao mahiri, Ally Yusuf ‘Tigana’.

Yusuf wakati wa enzi zake za kucheza soka ya ushindani alikuwa na uwezo mkubwa mno wa kuchezea mpira kama anavyotaka na kumudu kucheza vizuri dimba la kati, hali iliyowafanya mashabiki hao wa Manyema kumbatiza jina hilo la ‘Tigana’ wakimfananisha na Jean Tigana wa Ufaransa.

Msimu wa 1992/1993 klabu ya Nyota Nyekundu iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Pili baada ya kuona kipaji chake ilimsajili. Lakini pia msimu huo huo Pan African iliyokuwa ikishiriki ligi hiyo nao ilimsajili kwa dau kubwa zaidi kuliko timu ya awali Nyota Nyekundu, hivyo kutokana na kusajili timu mbili katika msimu mmoja, alifungiwa mwaka mmoja na kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT).

Licha ya nyota huyo kufungiwa, lakini msimu huo akawa anacheza mechi za kirafiki akiwa na Pan African. Baada ya adhabu yake ya mwaka mmoja kumalizika msimu wa 1993/1994 na baada ya Pan African kupanda Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu), Tigana alisajiliwa rasmi kuchezea timu hiyo yenye maskani yake makuu Mtaa wa Swahili chini ya mfadhili wao mkuu, Murtaza Dewji.

Tigana baada ya kujiunga rasmi na Pan African akawa ni mmoja wa wachezaji wa kutegemewa katika kikosi cha kwanza, huku akiwa na nyota wengine kama kipa Iddi Pazi ‘Father’, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, David Rodgers na Thomas Mashala.

Msimu wa 1994/1995 baada ya Dewji kutoka Pan African na kujiunga na Yanga, alimchukua nyota huyo na kuwa mmoja wa wachezaji wa kutumainiwa wa timu hiyo huku jina la Tigana likiendelea kuvuma na kuzoeleka.

Tigana akiwa na klabu hiyo ya Yanga alikuwa na wachezaji wengine chipukizi kama Anwar Awadh, Mzee Abdallah, Silvatus Ibrahim ‘Polisi’, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, Nonda Shabani na Maalim Saleh ‘Romario’.

Msimu wa 1996/1997, Tigana alihama Klabu ya Yanga na kujiunga na Simba huku jina hilo likiendelea kushamiri na ni msimu huo huo kutokana na kiwango cha juu cha soka alichokuwa nacho ndipo alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuchezea timu ya Taifa Stars.

Tigana pia akiwa na timu ya Taifa Stars jina hilo liliendelea kutumika. Alikaa na Klabu ya Simba misimu miwili na mwaka 1998 alitimkia nchini Mauritius kucheza soka la kulipwa katika timu ya Scouts Club akiwa na nyota kadhaa akiwemo Maalim Saleh ‘Romario’, Mwanamtwa Kiwhelo, Mohamed Hussein ‘Mmachinga na Shabani Ramadhani.

Mwaka 2000 Tigana alirudi nchini na kujiunga na Simba na mwaka uliofuata alijiunga tena na Yanga na kuichezea msimu mmoja na alistaafu kucheza soka ya ushindani mwaka 2004 akiwa na Klabu ya Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here