SHARE

kikosi cha yangaNA EZEKIEL TENDWA
JESHI lenye utimamu wa kimwili na kisaikolojia la mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, linatarajia kukwea pipa kesho kwenda nchini Rwanda tayari kwa mchezo wa raundi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR.
Kikosi cha Yanga chini ya Kocha Hans Pluijm kinaondoka huku kikiwa na ari kubwa ya kupata ushindi ugenini katika mchezo huo, utakaopigwa Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Amahoro, jijini Kigali.
Yanga wanakwenda ugenini kukipiga na Wanyarwanda hao wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi mnono waliopata kutoka kwenye Ligi Kuu dhidi ya African Sports ya jijini Tanga.
Yanga walianza kwa kishindo michuano hiyo hatua ya awali kwa kuitupa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0.
Kocha Pluijm ameliambia Dimba kwamba ameshanasa mbinu za APR, hivyo kazi iliyobakia ni jeshi lake kushambulia mwanzo mwisho ugenini.
Alisema, hana wasiwasi wowote na mchezo huo kutokana na jeuri ya kuwa na kikosi cha wachezaji wenye viwango vya kimataifa, hasa safu yake ya ushambuliaji, iliyo chini ya Donald Ngoma, Amis Tambwe, Malimi Busungu na Paul Nonga.
Alieleza katika safu yake ya kiungo yenye nyota Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima amewakabidhi jukumu la kuhakikisha wanapenyeza mipira hai kwa kina Ngoma na Tambwe ili kupata mabao ya kutosha tayari kwa kujiweka sawa na mchezo wa marudiano.

Pluijm anajua kuwa APR siyo timu ya kubeza, kwani inao wachezaji wazuri, akiwamo straika mahiri Meddy Kagere na Ndahinduka Michael, ambapo sasa akina Kelvin Yondani na Vicent Bossou wamepewa majukumu mazito kuhakikisha hawaruhusu mtu kupenya.
Akizungumzia ushiriki wao katika michuano hiyo, Pluijm alisema lengo lake ni kuhakikisha Yanga inafika mbali tofauti na misimu iliyopita na hilo linawezekana, kwani anacho kikosi chenye wachezaji wa kiwango cha juu.
“Kilichopo kwa sasa ni kuhakikisha tunafika mbali katika michuano hii, tumeanza kwa kuwatoa Cercle de Joachim, na kinachofuata ni kwa APR, najua kazi siyo rahisi, ila nawaamini wachezaji wangu na naamini watafuata kile ninachowafundisha kila siku,” alisema.
Baadhi ya mashabiki wa Yanga wamelazimika kufunga safari kuelekea nchini Rwanda kwa ajili ya kuwapa sapoti wachezaji wao kwenye mchezo huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here