SHARE

MANCHESTER, England

WAKATI Pep Guardiola akianza kuifanyia kazi safu yake ya ushambuliaji, ili ije kuzisumbua safu za ulinzi za wapinzani hapo baadaye, kuna huyu kijana wa Kibrazil aliye kwenye mpango huo kabambe wa Guardiola.

Anaitwa Gabriel Jesus.

Mwanzoni mwa msimum, Guardiola alianza vizuri mno, katikati hali ikabadilika lakini kutokana na ujio wa Mbrazil huyo huenda kibarua chake kikawa kimepata mwokozi.

Jesus alifanya kazi nzuri kwenye mchezo wa FA dhidi ya Crystal Palace na baada ya hapo akapewa nafasi ya kumaliza dakika 90 za mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu England dhidi ya West Ham, akifunga bao na kutoa ‘asisti’.

Guardiola anaamini kuwa straika huyo atafanya mengi makubwa, hasa kutokana na namna alivyokuja kwenye wakati mwafaka wa kumpa presha Sergio Aguero, ambaye ni straika bora EPL ndani ya miaka mitano ya hivi karibuni. Je, atafanikiwa?

Mtandao wa Daily Mail umechambua faida watakazozipata City kutokana na uwepo wa Jesus na changamoto itakayomkumba Aguero ndani ya kikosi hicho.

JICHO MAKINI GOLINI

Sifa mojawapo ya straika ni kuwa na jicho kali pindi afikapo kwenye goli la mpinzani, ajue ni wapi mpira unapotakiwa kutua na mlinda mlango asiweze kuucheza.

Tangu City ilipomnyakua Aguero kutoka Atletico Madrid, straika huyo amekuwa na rekodi nzuri ya ufungaji mabao ndani ya klabu hiyo.

Hadi sasa ‘Kun’ ameifungia City jumla ya mabao 113 ya kwenye mechi 146 za ligi tu.

Je, unajua ni kwanini wadau wengi wa soka huwa wanashangazwa kutoona straika huyo akitunukiwa tuzo kila mwisho wa ligi unapofika? Ni kutokana na uwezo wake mzuri wa kutupia mabao kila msimu ambao unawaaminisha kuwa si mtu wa kukosa tuzo hivi hivi.

Ndio maana hadi sasa hakuna anayekumbuka kuwa msimu huu ulianza vizuri mno kwa Aguero kupachika mabao 11 ndani ya mechi sita za awali, zikiwemo ‘hat trick’ mbili.

Sifa hiyo ya Aguero ipo kwa Jesus. Straika huyo aliyefunga mabao 21 kwenye msimu wake wa pili akiwa na Palmeiras kule Brazil, hakusajiliwa kuja kuuza sura England, bali alikuja kwa kazi moja tu, kufunga mabao. Na ameianza rasmi dhidi ya West Ham.

USUMBUFU KWA MABEKI

Je, unatambua ni kitu gani  kiliwashawishi City kutoa kiasi cha pauni milioni 27 kumsajili Jesus? Ni namna alivyo msumbufu kwa mabeki wa timu pinzani.

Jinsi anavyowapa mabeki kazi ya ziada na ‘kuwafosi’ wafanye makosa kwenye eneo lao wenyewe haina tofauti na washambuliaji waliowahi kucheza chini ya Guardiola kwenye klabu nyingine.

“Nikiwa dimbani ninapenda kuonekana kama mpambanaji,” Jesus analiambia jarida la FourFourTwo.

“Ninapenda kucheza soka la nguvu na kusukuma mashambulizi.

“Nilipoanza kucheza soka nilipenda kupambana na wakubwa zangu pamoja na mabeki wenye nguvu uwanjani. Siogopi kuchezewa rafu. Ninapenda ushindi na nitapambana ili tushinde.”

Hapo umegundua nini? Ipo tofauti baina ya Jesus na Aguero, tena kubwa mno.

Wakati Jesus akipenda soka la nguvu, kupambana zaidi, Aguero yeye uwezo wake wa kufunga utabaki pale pale lakini kwa mfumo wa Guardiola wa kukimbia zaidi hata wasipokuwa na mpira (kukaba kwa nguvu), Muargentina huyo huenda akajikuta akipoteza nafasi yake hivi hivi kwa dogo huyu!

KIRAKA

Jesus ametinga City huku akiwa bado mdogo lakini uwezo wake wa kucheza upande wowote kwenye safu ya ushambuliaji umemwezesha kuwa na uhakika wa nafasi yake kikosi cha kwanza muda wowote kuanzia sasa.

Aidha, straika huyo anaipa City nafasi nzuri ya kuwa na machaguo mengi ya ushambuliaji hasa akitokea pembeni kwa kasi.

Nafasi ya ushambuliaji wa kati itabaki kuwa ya Aguero, lakini bado Guardiola anasisitiza kuwa wapachika mabao hao wana uwezo wa kucheza pamoja pia.

“Watacheza pamoja, Jesus atakuwa akitokea pembeni na Aguero atabaki kuwa mchezaji muhimu kwetu. Hatuwezi kufikia malengo yetu bila ya mchango wake,” anasema Guardiola.

USHIRIKIANO

Zaidi ya yote, Jesus ameonesha kuwa na roho ya ushirikiano kwa wenzake.

Mabao matatu yaliyofungwa na City yalihusisha mashambulizi kupitia kwake, Leroy Sane, Raheem Sterling na Kevin De Bruyne.

Kutokana na hilo, inaonekana wazi kuwa Guardiola amekuwa akiwanoa vijana wake hao kushirikiana uwanjani kadiri wawezavyo.

Ushirikiano unaozungumziwa hapa ni zile pasi za mwisho kwenye eneo la adui, huenda akawa ni De Bruyne, Sterling au Silva ambaye ataitoa pasi hiyo lakini ni yeyote yule ana jukumu hilo kwenye mashambulizi.

Hadi sasa Jesus ana asisti mbili na bao moja, ndio kwanza amecheza mechi mbili (FA na ligi). Subirini mengi kutoka kwa huyu kijana, amekuja kuuwasha moto EPL.

Lakini zaidi ya kusubiri huo moto wa Jesus, mkae mkitambua kuwa amekuja kuanzisha vita kali ya namba na Aguero, tuusubiri mwisho wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here