SHARE

NA WINFRIDA MTOI

STRAIKA wa Yanga, Bernard Morrison, amevunja rekodi katika klabu hiyo baada ya mauzo ya jezi yake kuingiza zaidi ya Shilingi Mil. 250 za Kitanzania.

Kiasi hicho cha fedha kimetokana na mauzo ya jezi 5000 zenye jina na namba anayovaa Morrison zilizoandikwa BM 33 ambazo moja iliuzwa kati ya sh. 50,000 hadi 70,000.

Morrison alisajiliwa Yanga katika kipindi cha dirisha dogo kwa mkataba mfupi wa miezi sita, lakini baada ya kufanya vizuri uwanjani juzi, aliongezewa kandarasi ya miaka miwili.

Nyota huyo raia wa Ghana, amezidi kuleta vitu vya tofauti katika klabu hiyo, ikiwa ni pamoja na mtindo wake wa kuchezea mpira uwanjani jambo ambalo huvutia zaidi mashabiki.

Ukiangalia kiasi cha fedha kilichoingia kutokana na mauzo ya jezi yake, kinaweza hata kumlipa mshahara au kufanya usajili wa wachezaji wengine kikosini hapo.

Wapo wachezaji wengi waliopita Yanga kwa misimu ya hivi karibuni na kuwa vipenzi vya mashabiki, lakini hawajafikia rekodi ya mauzo ya jezi kwa kiwango hicho.

Mfano, nyota waliowahi kuwakuna Wanayanga, ni Donald Ngoma na Haruna Niyonzima ambaye amrejea tena, ila haijawahi kutangazwa jezi zao kuuzwa kwa bei kubwa na nyingi kiasi hicho kwa muda mfupi. 

Tangu Morrison ametua Yanga, ni miezi mitatu imekatika, hivyo kama ataendelea kung’ara kwa miaka miwili aliyosaini, kuna uwezekano akavunja rekodi zaidi.

Makamu Mwenyekiti wa Wanajangwani hao, Frederick Mwakalebela, amethibitisha Morrison kuuza idadi hiyo ya jezi na kufurahishwa na mafanikio hayo. 

Mwakalebela alisema jezi hizo zimeuzwa katika maduka mbalimbali na zinaendelea kuuzwa, wanatarajia idadi ya mauzo itaongezeka.

“Morrison ndiye mchezaji aliyeweka rekodi ya mauzo ya jezi kwa bei kubwa na wingi katika soka la Tanzania na wachezaji na klabu zote,” alisema Mwakalebela.

Alisema hiyo ni sifa kubwa kwa klabu yao, kwa sababu inakuwa inajitangaza na inachangia wachezaji wengine kujitumia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here