SHARE

WINFRIDA MTOI                                    

NI kweli mashabiki wa Yanga wameonyesha kwa vitendo nia ya kuunga mkono, ununuzi wa jesi zao, baada ya jana kuzishambulia na kuzifanya ziadimike mitaani.

Hali ilitokana na kugombewa na mashabiki wa timu hiyo kila mmoja akitaka kuanza kuivaa.

Jezi hiyo  inayotengenezwa na kusambazwa na   kampuni ya GSM, ilizinduliwa juzi kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, lakini hadi jana mtaani zilikuwa adimu, huku mashabiki wakihaha kuzitafuta.

Katika kuthibitisha hilo, wapenzi hao wa Yanga, walifurika makao makuu ya Klabu hiyo, maungio mitaa ya Twiga na Jangwani tangu asubuhi wakisubiri kuletwa jezi nyingine baada ya zile za awali, kuambiwa zimemalizika.

Mashabiki hao wa Wanajangwani walifurika klabuni baada ya kutangaziwa kuwa  ndiyo moja ya sehemu zitakazopatikana jezi hizo.

Mmoja wa mashabiki wa Yanga alijitambulisha kwa jina la Salim Khamis, alisema amefika eneo hilo  na kuambiwa jezi zimeisha lakini saa 9:00 jioni  mzigo mwingine ungewasili.

Hata hivyo baada ya muda huo kufika wakaambiwa watazipata leo uwanjani  litakapofanyika tamasha la Wiki ya Wananchi na pia kuchezwa mechi dhidi ya kariaobangi Skarks majira ya jioni.

 “Nataka kesho niende uwanjani nikiwa nimevaa jezi mpya, lakini nimekwenda madukani nimekosa, nikaambiwa makao makuu zinapatikana, nimekuja tumeimbiwa zimeisha  hadi kesho uwanjani,” alisema.

Tofauti na Makao Makuu ya Yanga, sehemu nyingine iliyotangazwa kuwa jezi hiyo itapatikana ni  katika maduka ya GSM ya Msasani Mall, Pugu Mall kabla ya kuanza kuuzwa maduka mengine jijini Dar es Salaam.

Jezi ambazo zinauliziwa sana na wapenzi hao wa Yanga ni zile zenye namba zinazovaliwa na nyota wapya, Juma Balinya, Maybin Kalengo na Lamine Moro.

Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Fredrick Mwakalebela, alikiri kuwepo kwa mahitaji makubwa ya jezi hiyo na kusema, klabu yake itahakikisha kila mshabiki anayehitaji ataipata.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here