Home Habari JJUUKO MIKONONI MWA YANGA

JJUUKO MIKONONI MWA YANGA

4112
0
SHARE

EZEKIEL TENDWA NA SAADA SALIM

FURAHA inayoendelea kwa mashabiki wa Simba ya kuingia kwenye mfumo mpya wa mabadiliko, inaweza ikakatika ghafla watakapopata taarifa hizi kwamba, Yanga wamewazunguka mlango wa nyuma na kumuingiza kwenye mikono yao beki kisiki Mganda, Jjuuko Murshid.

Taarifa za kina ambazo DIMBA Jumatano imepenyezewa, zinadai kuwa kigogo wao mmoja alikwenda Uganda akazungumza na beki huyo, mazungumzo ambayo yanatajwa kwenda vizuri kwa asilimia 70.

Beki huyo ambaye ndiye pekee aliyeitwa kwenye kikosi cha timu yake ya Taifa kinachoshiriki michuano ya Cecafa kwa wachezaji wanaocheza nje ya ligi yao, anatajwa kuwa mbadala wa Vincent Bossou aliyeikacha Yanga, japo kwa sasa anatamani kurudi.

Kigogo mmoja wa Yanga ameliambia DIMBA Jumatano kuwa, wamemtia mikononi mwao Jjuuko na kilichobakia na kumalizana tu na huenda siku chache zijazo wakamtangaza kuwa mchezaji wao kama Simba hawatashtukia mchezo uliochezwa na watani zao hao wa jadi.

“Yupo mtu wetu amekwenda Uganda akazungumza na Jjuuko kwa kina, kwa ujumla mazungumzo yalikwenda vizuri na kilichobakia ni kusaini tu, tunatarajia kufanya hivyo mapema kabla Simba hawajamshawishi abakie,” alisema kigogo huyo.

Hata hivyo, taarifa za kina zinadai kuwa, Mwenyekiti wao wa usajili, Hussein Nyika ndiye aliyekwenda Uganda kukutana na Jjuuko, ambapo inaelezwa walizungumza kila kitu na kukubaliana baadhi ya vipengele na kilichobakia ni kusaini tu.

DIMBA Jumatano lilipomtafuta Katibu Mkuu wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuzungumzia usajili wao kwa ujumla, alisema mwenyekiti wao wa usajili atakapowasili nchini ataweka kila kitu bayana.

“Msubiri Nyika akiwasili atakuwa na stori, siwezi kuweka wazi subiri, mpaka arejee labda anakuja na mchezaji kutoka Uganda unajuaje, kuwa na subira,” alisema Mkwasa akimaanisha kuwa mwenyekiti huyo wa usajili alikuwa nchini Uganda.

Taarifa zaidi zinadai kuwa huenda Jjuuko asiwe na kipingamizi cha kutua Yanga, kwani licha ya uwezo mkubwa alionao, lakini amekuwa akijikuta anasugulishwa benchi Simba, kitu ambacho kiliripotiwa kumkera aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Uganda, Millutin Micho.

Jjuuko ni mmoja wa mabeki ambao hawana masihara wanapokuwa uwanjani, ambapo kama Yanga watafanikiwa kuinasa saini yake, watakuwa wamelamba dume, wakiacha kilio kwa wapinzani wao hao wa jadi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here