SHARE

NA MWAMVITA MTANDA

HII kasi ya kupachika mabao anayokwenda nayo straika wa Simba, Meddie Kagere, usidhani inawanufaisha Wanamsimbazi tu, hata yeye mwenyewe anajiwekea uhakika wa kula bata katika siku za usoni.

Mpaka sasa spidi ya Mnyarwanda huyo inatishia kuvunja rekodi aliyoiweka msimu uliyopita alipofunga mabao 23 na kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara.

Tayari hadi sasa ameshaweka kimiani mabao sita katika michezo minne tu aliyoichezea timu yake hiyo aliyojiunga nayo msimu uliopita akitokea Gor Mahia ya Kenya.

Zali lililopo mkononi mwa Kagere kwa sasa ni kupata nafasi ya kucheza nchini Marekani, endapo atatimiza masharti mepesi ambayo yanaonyesha wazi kwamba atayamudu.

Meneja wa mchezaji huyo, Patrick Gakumba, akizungumza na DIMBA Jumatano kutoka Kigali nchini Rwanda, alisema amevutiwa na juhudi anazoonyesha mchezaji wake na hivyo ameamua kumuwekea ofa nzuri mbele yake aliyoipata kutoka nchini Marekani.

Akaongeza kuwa amepokea ujumbe kutoka Dallas FC ya Marekani wakionyesha nia ya kumhitaji mcheza kutoka Afrika ambaye ni Kagere, lakini sharti lake ni kutimiza idadi ya mabao 25 ili aweze kukidhi vigezo vya kujiunga na timu hiyo.

Meneja huyo alisema kwa sasa jina la Kagere limesambaa karibu dunia nzima kutokana na juhudi anazoonyesha katika ukanda huu waAfrika Mashariki, kiasi cha kupokea simu kutoka kila upande wakihitaji huduma yake.

Gakumba ana uhakika kwamba Kagera anaweza kufikisha idadi hiyo ya mabao mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara na kuendelea kumpa imani kwamba hiyo ofa tayari ipo mikononi mwake.

Pia alidokeza kwamba, endapo mipango hiyo itakwenda kama alivyopanga basi mchezaji wake atavuna dau nono zaidi ya mara nne ya lile alilopata alivyosaliwa Msimbazi.

“Hata hivyo najua kwa sasa Kagere ni mali ya Simba, nawasiliana naye nikimtaka azidi kuitumikia klabu hiyo kwa nguvu zote huku akikumbuka deni la mabao 25 linalohitajika.

Mpaka sasa Kagere ni kama ameanza kuikimbiza vita ya kugombea ufungaji bora Ligi Kuu Bara kutokana na kuwatangulia wenzake ambapo hadi sasa ana mabao matatu zaidi ya straika mwenzake wa Simba, Miraji Athumani.

Wanaofuatia ni Yusufu Mhilu (Kagera Sugar), Jerry Tegete (Alliance), Awesu Awesu (Kagera Sugar), Sadaat Mohamed (Ruvu Shooting), Paul Nonga (Lipuli) na Peter Mapunda wa Mbeya City ambao wote wamefunga mabao mawili kila mmoja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here