SHARE

NA ZAINAB IDDY
KINARA wa kucheka na nyavu katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Meddie Kagere ametumia dakika 450 za ukame kabla ya kuziona nyavu katika mechi za Ligi Kuu baada ya jana kutupia dhidi ya Kagera Sugar.
Kagere aliyekuwa mfungaji bora msimu wa Ligi Kuu uliopita akiwa na mabao 23, hivi sasa amefunga 13 na kuongoza katika ufungaji akifuatiwa na Yusuph Mhilu wa Kagera Sugar mwenye mabao 9.
Mara ya mwisho Kagere kuziona nyavu za wapinzani ilikuwa katika mchezo wa Simba dhidi ya Namungo FC ambao Wanamsimbazi walishinda mabao 3-2 mchezo ukipigwa ndani ya dimba la Taifa, Dar es Salaam.
Tangu hapo Simba imecheza michezo mitano ambayo nyota huyo ameshindwa kufunga ingawa aliweza kuasisti bao moja lililofungwa na John Bocco katika mchezo na Mtibwa Sugar uliochezwa uwanja wa Jamhuri,Morogoro na kumalizika kwa Wekundu wa Msimbazi kushinda 3-0.
Katika kipindi ambacho Kagere alikuwa kwenye ukame wa mabao Simba imeweza kuvuna mabao nane katika michezo mitano iliyocheza kabla ya mechi ya jana dhidi ya Kagera Sugar.
Katika michezo hiyo, Simba iliweza kuichapa Coastal Union (2-0), wakaja kuwatandika Polisi Tanzania (2-1) kabla ya Wekundu wa Msimbazi kufungwa (1-0) na JKT Tanzania.
Vinara hao wa ligi walisafiri hadi mkoani Morogoro na kuwatandika 3-0 Mtibwa Sugar kisha wakawachapa 1-0 Lipuli FC ya mjini Iringa na kurejea jijini Dar es Salaam kucheza na Kagera Sugar jana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here