Home Habari KAGERE AWEKA REKODI 3 SIMBA

KAGERE AWEKA REKODI 3 SIMBA

1616
0
SHARE

NA MAREGES NYAMAKA


STRAIKA hatari wa Simba, Meddie Kagere ‘MK14’, aliyeanza kwa kasi ya ajabu ya kupachika mabao katika michuano ya Ligi Kuu msimu wa 2018/19, kama masihara vile ameshatengeneza rekodi tatu katika klabu yake hiyo aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya.
Juzi straika huyo alikuwa chachu ya ushindi wa Wekundu hao wa Msimbazi walipowatungua Mbeya City mabao 2-0, yote akifunga yeye katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Ulikuwa ni mwendelezo wa mechi ya pili mfululizo katika ligi hiyo, huku Kagere akifumania nyavu, kwani alianza kufanya hivyo mchezo wa ufunguzi dhidi ya Prisons uliomalizika kwa ushindi wa bao 1-0 na kumfanya kuweka rekodi tatu hatari kwenye ligi hiyo yenye jumla ya timu 20.

Rekodi ya kwanza ni ile ya straika huyo aliyekuwa Gor Mahia ya Kenya kufunga mabao mawili kwa staili moja ya vichwa, la kwanza akitumia krosi ya Shiza Kichuya pamoja na ya Asante Kwasi.
Ya pili aliyoweka Mganda huyo ni kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la mapema kuliko mchezaji yeyote, akifanya hivyo dakika ya pili alipowatungua Tanzania Prisons, akifuatiwa na Salum Ijee wa Mwadui aliyefunga daki ya tisa.

Lakini pia Kagere, ambaye Simba ni timu yake 11 kuichezea tangu aanze kucheza soka la ushindani, ni straika pekee aliyefunga mabao mengi hadi sasa, ambayo ni tisa kwa mechi zote, zikiwamo za kirafiki ndani ya kikosi hicho.
Mbali na mabao matatu ya ligi hiyo yanayomfanya kuongoza msimamo wa wafungaji, nyota huyo aliingia kimiani mara tano katika michuano ya Kagame, dhidi ya timu za APR ya Rwanda, Singida United, JKU na Azam.
Mechi nyingine alizofunga ni dhidi ya Mtibwa Sugar mechi ya Ngao ya Jamii, katika ushindi wa mabao 2-1 pamoja na mchezo wa kirafiki mbele F.C.E Kasaifa, walipokuwa kambini nchini Uturuki wakiibuka na ushindi wa mabao 3-1, mawili yakifungwa na Emmanuel Okwi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here