SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

KAMA ulidhani baada ya Emmanuel Okwi, kuondoka Simba, kuna kitu kitakachoharibika hasa kwenye safu ya ushambiliaji, basi utakuwa hujui kinachoendelea huko Afrika Kusini walikiweka kambi Wekundu hao wa Msimbazi.

Simba wameweka kambi kwenye hoteli ya Royal Marang katika Mji wa Rustenburg, ikiwa ni maandalizi yao ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Kimataifa.

Uongozi wa Simba na benchi lao la ufundi wanajua kazi kubwa waliyonayo ni kuhakikisha wanatetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara lakini pia kufika mbali zaidi Ligi ya Mabingwa Afrika, ndiyo maana wakaamua kufanya usajili mkubwa na kwenda kujificha Afrika Kusini.

Katika usajili huo jina la Emmanuel Okwi, halipo baada ya kutofikia makubaliano na uongozi, lakini hilo sio tatizo kwani zimeongezwa mashine nyingine ambazo tayari zimeshaanza kutengeneza kombinesheni ya kutisha kwenye safu ya ushambuliaji.

Okwi, Meddie Kagere pamoja na John Bocco, walikuwa hatari sana kwenye safu hiyo ya ushambuliaji msimu uliopita wakifunga mabao ya kutosha lakini sasa mambo yamebadilika na kinachoonekana ni kwamba msimu ujao ndiyo itakuwa hatari zaidi.

Licha ya kwamba Okwi hatakuwepo lakini usajili wa Deo Kanda, umeonekana kujibu maswali waliyonayo mashabiki wengi kutokana na namna alivyotengeneza ushirikiano nzuri, yeye na Kagere pamoja na Bocco na kumfanya kocha wao Mkuu Patrick Aussems, kuamini kwamba hakuna timu itakayopona mbele yao.

Washambuliaji hao wametengeneza ‘utatu mtakatifu’, huku Ibrahim Ajib naye akionyesha makeke yake, hiyo ikimaanisha kuwa kazi kubwa kwa benchi la ufundi itakuwa ni kupanga mchezaji wa kuanza na na wale wa kusubiri.

Simba wanafanya mazoezi makali huku wakijua kwamba watani zao wa jadi Yanga, wapo kikazi zaidi wakijichimbia mjini Morogoro, kuhakikisha msimu ujao wanalirejesha kombe mikononi mwao baada ya ‘kulimisi’ kwa misimu miwili.

Mbali na kutaka kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, pia Wekundu hao wa Msimbazi wanajua kwamba wanatakiwa kupiga hatua nyingine mbele Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya msimu huu kuishia hatua ya robo fainali.

Kwa mujibu wa ratiba waliyoitoa, Simba watakuwa na michezo minne ya kirafiki wakianza dhidi ya Orbret TVET, Jumanne ya wiki inayokuja na siku inayofuata watakipiga dhidi ya Platinum Stars zote za Afrika Kusini.

Julai Julai 27 watacheza dhidi ya Township Rollers ya Botswana ambayo iliwahi kuifunga Yanga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2018 na Julai 30 watamaliza dhidi ya Orlando Pirates.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here