SHARE

NA TIMA SIKILO

BAADA ya kuiongoza timu yake kutinga hatua ya fainali huku akionyesha uwezo mkubwa ikiwemo kupangua mkwaju mmoja wa penalti dhidi ya Azam FC, kipa wa Simba, Beno Kakolanya, amesema anapata ushirikiano mzuri na makipa wenzake ndiyo maana anafanya kazi nzuri.

Kakolanya ndiye aliyesimama langoni katika mchezo wa nusu fainali wa michuano ya Mapinduzi dhidi ya Azam FC wakishinda mabao 3-2 kwa mikwaju ya penalti huku kipa huyo akiokoa mchomo mmoja wa mwisho.

Kipa huyo alidaka penalti ya mwisho iliyopigwa na kipa mwenzake wa Azam FC, Razack Abalora, huku penalti ya Donald Ngoma ikipaa na ile ya Idd Kipagwile ikigonga mwamba na kurudi uwanjani.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kakolanya alisema makipa wote waliopo Simba ni wazuri ndiyo maana kila anayepangwa mambo yanakwenda vizuri huku akiwaomba mashabiki kuendelea kuwapa sapoti.

“Simba ina makipa wazuri na yeyote anayepangwa anafanya kazi vizuri, kilichopo ni mashabiki kuendelea kutuunga mkono katika harakati zetu za kuipatia timu mafanikio,” alisema.

Nyota ya Kakolanya iliibuka zaidi msimu uliopita alipokuwa akiitumikia Yanga hasa mchezo wa mzunguko wa kwanza ambapo aliokoa michomo mingi ya washambuliaji wa Simba na kuufanya mchezo kumalizika kwa suluhu ya 0-0.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here