SHARE

Kali OngalaNA ZAINAB IDDY

UKISIKIA zali ndilo hili. Kocha Mkuu wa Majimaji, Kali Ongala, amegeuka dili baada ya timu hiyo kutaka kumwongezea mkataba huku African Lyon ambayo imepanda daraja ikimhitaji kwa kila hali.

Akizungumza na DIMBA jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Majimaji,  Humphrey Milanzi, alisema kwa sasa wapo kwenye mazungumzo ya mwisho mwisho na kocha huyo na tayari wamemwekea mkataba mezani na unapitiwa na mwanasheria wake.

“Nipo jijini Dar es Salaam nimemletea mkataba kocha wetu na sasa hivi upo mikononi mwa mwanasheria wake anaupitia, nina imani tutamalizana naye kadiri inavyowezekana,” alisema Milanzi.

Kwa upande wake African Lyon, Mkurugenzi wa klabu hiyo, Rahim Kangezi Zamunda, alisema walizungumza na Ongala kwa ajili ya kumkabidhi majukumu lakini bado hawajafikia mwafaka.

“Kwa ujumla tumefanya naye mazungumzo ya awali kwani tumeridhishwa na uwezo wake ila mambo bado hayajakaa sawa, yeye anataka dau kubwa ndiyo maana mpaka sasa hatujamalizana,” alisema.

Ongala nyota wa zamani wa Kajumulo na Yanga zote za Dar es Salaam, amemaliza mkataba wake na Majimaji na sasa wamemwekea mwingine mezani lakini wakati wanaendelea na mazungumzo hayo, African Lyon nao wameingilia kati wakitaka kumnyakua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here