SHARE

MUNICH, Ujerumani


JUZI ilikuwa siku mbaya kwa staa wa tenisi, mwanadada raia wa Ujerumani, Angelique Kerber, baada ya kuondoshwa na Kristina Mladenovic wa Ufaransa katika michuano ya US Open.


Licha ya uzoefu wake, Kerber aliyewahi kushika nafasi ya kwanza katika orodha ya ubora duniani, alijikuta akisukumwa nje ya mashindano hayo kwa kichapo cha seti 7-5, 0-6, 6-4.


Inafahamika kuwa Kerber alikuwa bingwa wa Australian Open mwaka 2016 na mwaka jana ulikuwa mzuri kwake pia kwa kulipeleka nyumbani taji la Wimbledon.


Hii inakuwa mara ya kwanza kumshuhudia Kerber akifungwa katika raundi ya kwanza kwa michuano mitatu mfululizo iliyopita.

Aliikataa Poland kisa Ujerumani
Kerber angeweza kuiwakilisha Poland katika michuano ya kimataifa kwa kuwa huko ndiko walikotokea wazazi wake. Hata hivyo, alizaliwa Ujerumani na kuamua kuipeperusha bendera ya taifa hilo.


Katika mahojiano yake, anasema ni kweli ana ukaribu mkubwa na Poland lakini huwa anajisikia furaha zaidi kutambulika kwa uraia wa Ujerumani.

Baba, bibi walimtoa kiaina
Kipaji chake hakikuwa cha kubahatisha kwani anatokea familia ya mchezo huo, ikielezwa kwamba huko mjini Puszczykowo, Poland, babu na bibi yake walikuwa wakimiliki ‘academy’ ya mchezo huo na hadi leo ipo.


Pia, baba yake mzazi, Slamowir Kerber, naye alikuwa mkali wa tenisi na ndiye aliyekuwa kocha wake wa kwanza wakati anaanza safari ya mafanikio aliyonayo sasa.

Humwambii kitu kwenye soka
Kerber, licha ya kwamba ni tenesi ndiyo inayompa ‘ugali’ na umaarufu alionao, yeye ni shabiki mkubwa wa mchezo wa mpira wa miguu.


Nyota huyo anayetumia mkono wa kushoto, anaitaja Bayern Munich kuwa ndiyo timu ya soka anayoishabikia tangu alipoanza kuwa na mapenzi na mchezo huo.


Kiboko ya Serena
Kwanza, hadi leo hii, Kerber anaheshimika Ujerumani kwa kuwa ndiye mchezaji tenisi pekee wa kike kutwaa ubingwa wa michuano ya Wimbledon baada ya nchi hiyo kusubiri kwa kipindi cha miaka 20.
Aidha, bibiye huyo anaingia kwenye orodha ya mastaa wawili pekee wa mchezo wa tenesi kuwafunga Serena na Venus Williams mara mbili katika mchezo wa fainali ya michuano mikubwa (Grand Slam).

Hii ya Kerber kali kweli
Ni kawaida ya wachezaji wa tenisi kuwa na wasaidizi wao mazoezini, ambao hufanya kazi ya kuwaokotea mipira. Iko hivyo kokote na kwa mastaa wengi wa mchezo huo.
Hata hivyo, usidhani kwa Kerbers iko hivyo. Anatajwa kuwa ni staa wa tenesi pekee ambaye mazoezini huokota mipira mwenyewe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here