SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

WINGA wa Simba, Shiza Kichuya na straika wa Yanga, Obrey Chirwa, mikataba yao na timu zao inakwisha mara baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi, na kama ulivyo ule msemo wa kisasa, mara paap!, huenda wawili hao wakapishana mmoja akaenda huku na mwingine kule.

Wawili hao wataruhusiwa kuanza kufanya mazungumzo na timu yoyote itakayowahitaji kuanzia mwishoni mwa mwezi ujao, kwani mikataba yao kila mmoja itabakia miezi sita.

Kocha Mkuu wa Yanga, yenye makazi yake mitaa ya Twiga na Jangwani, George Lwandamina, hivi karibuni aliuambia uongozi wa timu hiyo kuwa, anaweza kuifanya timu hiyo ikatetea ubingwa wake kwa mara ya nne mfululizo na pia kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa, lakini kama tu uongozi huo utafanyia kazi mapendekezo yake kuanzia kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

Moja ya mapendekezo yake ni kutafutiwa winga mmoja wa kushoto mwenye kasi kubwa zaidi ya aliyokuwa nayo Simon Msuva, lakini pia mwenye sifa nyingine ya kumudu kucheza kama kiungo wa kati.

Licha ya kuwa mawinga kama Geofrey Mwashiuya, Emmanuel Martin pamoja na Pius Buswita, kocha huyo anaona bado kuna kitu kinakosekana, hivyo amependekeza atafutwe mwingine matata anayetumia mguu wa kushoto, ambaye atakuwa akimtumia kuanzishia mashambulizi.

Ingawa hakumtaja hadharani ni mchezaji gani, lakini kuna tetesi zinazagaa chini kwa chini kuwa huenda akawa ni winga wa Simba, Kichuya.

Kichuya mwenyewe hivi karibuni alikaririwa akisema bado hajafikia uamuzi wa kusaini mkataba mpya na klabu hiyo kwa sababu ya kuangalia maslahi kwanza.

Alisema bado yeye na meneja wake hawajafikia uamuzi wa kusaini klabu yoyote mpaka sasa kwa sababu wanataka kuona mkataba mpya unakuwa na maslahi bora kuliko alichokuwa anapata sasa.

Kichuya, aliyesajiliwa na Simba msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar, alisema yeye atakuwa tayari kusaini mkataba ambao utamridhisha, bila kujali klabu itakayomvutia, iwe ya ndani au nje ya Tanzania.

“Bado sijafanya uamuzi wowote kuhusu kusaini mkataba mpya, nitamsikiliza meneja wangu kile ambacho ataniamulia,” alisema kwa kifupi nyota huyo anayevaa jezi namba 25 mgongoni.

Kwa upande wa Chirwa, ingawa Wekundu hao wa Msimbazi hawajasema lolote kuhusu nia yao ya kutaka kumsainisha, lakini kocha wa timu hiyo, Joseph Omog, amesema kwamba, anahitaji straika mpambanaji mwenye uwezo kama alionao Mzambia huyo.

Inadaiwa kwamba, Simba wako mbioni kumtema kiungo Mrundi Laudit Mavugo, ambaye anaonekana kushindwa kuonyesha makeke aliyokuwa nayo Vital’O ya Burundi, na sasa wanamtafuta mbadala wake ambaye atakuwa ni straika wa kigeni.

Taarifa zinadai kuwa, wanaweza kumpata Chirwa ‘kiulaini’ mara baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu wa ligi.

Habari zinasema mara mkataba wake utakapomalizika, Yanga huenda ikaachana naye kutokana na sababu kuu mbili; moja ikiwa hali mbaya ya kifedha iliyonayo klabu hiyo na mbili ni ukubwa wa mshahara wake ambao Yanga huenda wakashindwa kuulipa.

Chirwa, aliyesajiliwa na Yanga kutoka FC Platinum ya Zimbabwe kwa dau la zaidi ya Sh milioni 200 za Kitanzania na kusaini mkataba wa miaka miwili, anayelipwa takriban Sh milioni kumi za Kitanzania kwa mwezi, mkataba wake utakwisha Juni mwakani.

Iwapo Yanga watamuachia, Kocha wa Simba, Joseph Omog, hatakuwa na shida ya kusaka straika wa kigeni wa kumsajili zaidi ya Chirwa kutokana na kiwango anachokionyesha na klabu yake hivi sasa.

Lakini pia na wao Simba, kama watachelewa kumwongezea mkataba Kichuya, yanaweza yakawakuta kama ilivyokuwa kwa Ajib, huku Yanga wakiweza kukutana na yaliyowakuta ya Haruna Niyonzima.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here