Home Habari KIGOGO SIMBA AMTEKA NGOMA

KIGOGO SIMBA AMTEKA NGOMA

3303
0
SHARE

CLARA ALPHONCE NA SAADA SALIM

MASHABIKI wa Yanga wakisikia hii wanaweza wakawaona Simba wana roho mbaya sana, kwani wakati wao wakimsubiri kwa hamu straika wao Mzimbabwe, Donald Ngoma, kumbe kuna kigogo wa Wekundu wa Msimbazi, mwenye fedha zake, anawasiliana naye kila siku akiamini kwamba anaweza akamfanya avae jezi nyekundu na nyeupe zinazotumiwa na timu hiyo.

Taarifa za uhakika zilizolifikia DIMBA zinadai kuwa, kigogo huyo amekuwa na mawasiliano ya karibu na Ngoma, ndiyo maana Mzimbabwe huyo anakuwa na jeuri kwa waajiri wake, ili wamteme aweze kutua kirahisi kwa Wekundu hao wa Msimbazi.

Kigogo huyo, ambaye fedha kwake si shida, anataka kutumia mwanya huu wa wachezaji wa Yanga kucheleweshewa mishahara mara kwa mara kumnasa Ngoma, ndiyo maana taarifa hizo zinadai kuwa urafiki wao umekuwa mkubwa zaidi.

Hata kwa wakati huu Ngoma akiwa kwao Zimbabwe, inasemekana anawasiliana na kigogo huyo, lengo kubwa likiwa kutafuta namna ya kumvuta kwenye timu yao ili aungane na mwenzake, Haruna Niyonzima, aliyetua mwanzoni mwa msimu huu wa ligi.

Kigogo huyo ambaye jina lake kwa sasa bado tunaliweka kapuni, hakuweza kupatikana ili kuzungumzia suala hilo, lakini DIMBA liliamua kumuuliza Katibu Mkuu wa Simba, Arnold Kashembe, kama ana taarifa hizo, ambaye alisema yeye anachokijua ni kwamba mchezaji huyo bado ana mkataba na Yanga, na kwamba wao wanaliheshimu hilo.

“Ngoma ni mchezaji mzuri, lakini naamini bado anao mkataba na Yanga, hivyo tunaliheshimu hilo, nadhani kwa mengi unaweza kuzungumza na kamati husika ya usajili iliyopo chini ya Mwenyekiti wake, Zacharia Hans Poppe,” alisema.

Jitihada za kumpata Poppe zilishindikana, kwani simu yake ilikuwa haipatikani na taarifa zaidi zinadai kuwa kigogo huyo yupo nje ya nchi.

Kwa upande wao Yanga, kupitia kwa Mwenyekiti wa Usajili, Hussein Nyika, wamesema mchezaji huyo hawezi kwenda popote, kwani wana mkataba naye na kwamba wamewasiliana naye na wiki inayoanza kesho atarejea ili kujiunga na wenzake baada ya kumaliza matibabu.

“Tumewasiliana na dokta wake wa Zimbabwe, ametuambia anaendelea vizuri na yupo katika matibabu ya mwisho, wiki ijayo atatua kujiunga na wenzake kwa ajili ya michezo inayotukabili,” alisema Nyika.

Alisema hivi karibuni kamati yake na uongozi wa Yanga walikutana kujadili masuala mbalimbali ya usajili, ila ajenda ya kukata baadhi ya wachezaji ambao wameonekana mizigo na majeruhi sugu, haikufikia mwafaka, hivyo hakuna lolote lililoamuliwa juu ya hilo.

Awali Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema watampa adhabu mshambuliaji huyo kutokana na utovu wa nidhamu alioonyesha, baada ya kwenda kwao bila kupata baraka zao.

Hata hivyo, licha ya viongozi hao kusema anarejea wiki ijayo, DIMBA linafahamu kuwa, wameamua kunywea baada ya kusikia baadhi ya viongozi wa Simba wapo karibu sana naye, wakihofia asije akaenda kwa wapinzani wao hao kirahisi.

Katika dirisha kubwa la usajili Ngoma alikuwa akitajwa kujiunga na Simba kama mwenzake, Haruna Niyonzima, lakini Yanga ikazima uvumi huo baada ya kumsainisha mkataba wa miaka miwili.

Hata hivyo, msimu huu ulipoanza, Ngoma alicheza michezo michache kabla ya kukumbwa na majeraha na baadaye akaondoka kwenda kwao Zimbabwe, huku uongozi ukidai kuwa, hakutoa taarifa na kwamba adhabu kali inamngoja, lakini sasa wenyewe wamesema anarejea wiki ijayo kiroho safi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here