SHARE

LONDON, England

UNAIONA hiyo picha ya kikosi hapo? Unaambiwa hicho ndicho kikosi cha dhahabu cha England katika kipindi cha miaka 20 sasa.

Chini ya kocha Sven-Goran Eriksson, wanaume hawa 11 wa England walikuwa katika Jiji la Coimbra, Ureno kucheza mchezo wa pili wa makundi dhidi ya Uswisi, kwenye fainali za Euro 2004.

Kwenye pambano hilo, England waliibuka na ushindi wa mabao 3-0, Wayne Rooney, akiwa na miaka 18 alifunga mara mbili kabla ya Steven Gerrard kupigilia msumari wa mwisho.

Huku wengi wakiamini England wangefanya maajabu kwenye Euro, safari yao ilikatishwa na wenyeji, Ureno kwenye robo fainali baada ya kutandikwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Miongoni mwa nyota waliounda kikosi hicho ni nahodha wa zamani wa Chelsea, Frank Lampard, aliyetangaza kustaafu soka wiki hii akiwa na miaka 38.

Achana na Lampard, unajua walipo nyota wengine wa kikosi kile cha dhahabu cha England? Makala haya yanakupa majibu ya swali hilo.

DAVID JAMES 

James, kipindi hicho akiwa kipa wa Manchester City, aliibuka kuwa kipa namba moja wa England baada ya mkongwe, David Seaman, kustaafu.

Aliitwa kwa mara ya kwanza mwaka 2010 na kufanikiwa kucheza michezo 53, kabla ya kustaafu soka.

Mchezo wake wa mwisho aliucheza katika ligi ya India akiwa na klabu ya Kerala Blasters, ambapo baadaye aliifundisha kama kocha.

James ambaye amewahi kucheza katika klabu za Liverpool, Aston Villa na West Ham, hivi sasa ni mchambuzi kwenye kituo cha BT Sport.

GARY NEVILLE 

Beki huyu wa zamani wa Manchester United amecheza michezo 85 akiwa na jezi ya timu ya taifa.

Mara ya mwisho kucheza timu ya taifa ni mwaka 2007 na kwa upande wa klabu, mwaka 2011 ndio aliachana na Manchester United, akiwa na rekodi ya kubeba mataji nane ya Premier League, matatu ya Kombe la FA, mawili ya Kombe la Ligi na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Pia Neville amefanikiwa kuingia kwenye kikosi bora cha ligi mara tano.

Baada ya kustaafu, Neville aliingia kwenye kazi ya ukocha kabla ya kuanza uchambuzi katika kituo cha Sky Sports.

SOL CAMPBELL 

Bonge la beki aliyeiongoza Arsenal kucheza msimu mzima bila kufungwa na kuiongezea uimara safu ya ulinzi ya England kwenye fainali za Euro 2004 mpaka hatua ya robo fainali.

Campbell amecheza mechi 73 akiwa na England na alikuwepo kwenye kikosi kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia, mwaka 2006 nchini Ujerumani.

Baada ya kustaafu mwaka 2012, Campbell alijiunga kwenye masuala ya siasa kabla ya kupokea cheti cha ukocha na sasa ni kocha msaidizi wa taifa la Trinidad &Tobago.

JOHN TERRY

Terry na Campbell waliunda safu ngumu ya ulinzi ya England wakati nahodha huyu wa Chelsea akipata mafanikio na klabu yake chini ya kocha, Jose Mourinho.

Amecheza michezo 78 akiwa na kikosi cha ‘Three Lions’ na anabaki kuwa nyota muhimu kwenye kikosi cha dhahabu cha England.

Terry, kwa sasa ana miaka 36 na bado anaendelea kukipiga akiwa na Chelsea na inavyoonekana mkongwe huyu amebakiza misimu michache ya kuendelea kutumika uwanjani.

ASHLEY COLE

Kama ilivyokuwa Campbell, beki huyu wa kushoto alikuwemo kwenye kikosi cha Arsenal kilichotwaa ubingwa wa Premier League mwaka 2004.

Mwaka 2006 aliitikisa dunia alipohama Arsenal na kujiunga na matajiri wa London, Chelsea. Uhamisho huu ulimwongezea idadi ya mataji kwenye kabati lake.

Katika kipindi cha mwaka 2001 hadi 2014, Cole amecheza mechi 107 akiwa na jezi ya England na kuweka rekodi ya kuwa beki aliyecheza michezo mingi zaidi katika historia ya taifa hilo.

Cole, kwa sasa ana miaka 36, anakipiga katika klabu ya Los Angeles Galaxy inayoshiriki Ligi Kuu nchini Marekani.

DAVID BECKHAM

Nahodha wa England kwenye fainali za Euro 2004, alicheza mechi zote za michuano hiyo na mkosi pekee alioupata ni kuingia kwenye orodha ya waliokosa penalti kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Ureno.

Mpaka mwaka 2009 alipoachana na England, Beckham alicheza mechi 115 akiwa na jezi ya taifa hilo.

Nyota huyu wa zamani wa Manchester United, Real Madrid, AC Milan, PSG na LA Galaxy, kwa sasa ni balozi wa shirika la UNICEF.

STEVEN GERRARD

Injini muhimu ya England kwenye fainali za Euro 2004.

Kwa kipindi chote alichovaa jezi ya taifa la England, Gerrard amekuwa sehemu muhimu ya kikosi kwa kufunga na kutengeneza mabao.

Mpaka anaachana na timu ya Taifa akiwa amecheza michezo 114, kiungo huyu alikuwa na rekodi ya kuiongoza klabu yake ya Liverpool kubeba taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2005.

Gerrard alistaafu rasmi soka mwaka jana akiwa na klabu ya LA Galaxy inayoshiriki Ligi Kuu nchini Marekani, hivi sasa ni kocha wa vijana wa Liverpool.

FRANK LAMPARD

Mpaka leo dunia imebaki na swali la kwanini Steven Gerrard na Frank Lampard hawakuweza kucheza pamoja na kupata mafanikio wakiwa na jezi ya taifa la England.

Lampard amecheza mechi 106 akiwa na England, akifunga mabao 29, aliachana rasmi na taifa hilo mwaka 2014.

Ni mwaka huo pia alioachana na klabu ya Chelsea na kujiunga na Manchester City alipocheza kwa mkopo akitokea klabu ya New York City inayoshiriki Ligi Kuu nchini Marekani.

PAUL SCHOLES

Amini usiamini, fainali za Euro 2004 ndio zilikuwa za mwisho kwa mkali huyu wa mashuti ya mbali kucheza timu ya taifa ya England.

Alitangaza kustaafu akicheza michezo 66 tu na jezi ya timu ya taifa na kuamua kujikita zaidi na klabu yake ya Manchester United.

Akiwa na United, Scholes amecheza mechi zaidi ya 700 na kufanikiwa kutwaa mataji 11 ya Premier League, matatu ya Kombe la FA, mawili ya Kombe la Ligi na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Baada ya kustaafu mwaka 2013, Scholes alianza rasmi kazi ya uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya runinga.

MICHAEL OWEN

Zilikuwa fainali za nne kubwa kwa Owen akiwa na kikosi cha England na ulikuwa msimu ambao aliamua kuitema Liverpool na kujiunga na Real Madrid.

Owen amekuwa na rekodi bora ya ufungaji kwa ngazi ya klabu na taifa, akifunga mabao 40 kwenye michezo 89 aliyocheza akiwa na ‘Three Lions’.

Baada ya kustaafu soka, Owen aliingia kwenye kazi ya uchambuzi wa soka.

WAYNE ROONEY

Kijana mdogo kabisa wa klabu ya Everton, aliingia kwenye vichwa vya habari baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wa ufungaji kwenye fainali za Euro 2004.

Uwezo aliouonyesha kwenye fainali hizo ulimfanya kocha wa Man United, Sir Alex Ferguson, kuvunja benki na kumsajili.

Rooney kwa sasa ni nahodha wa England na Manchester United, amefanikiwa kuweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa taifa na klabu.

Mpaka sasa bado yuko Manchester na kumekuwa na tetesi nyingi za mkali huyu kutakiwa na klabu za China.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here