SHARE

Mbrazil awaongezea kasi Wabrazil

NA WINFRIDA MTOI

KILA idara ndani ya kikosi cha Simba sasa ni moto, kiasi cha kusema hivi sasa kazi iliyopo mbele yao ni kushusha vipigo tu katika mechi zao za Ligi Kuu Bara.

Hiyo imetokana na kauli ya kocha mkuu wa kikosi hicho, Patrick Aussems, aliyebainisha kwamba tayari amerekebisha safu yake ya ulinzi na kuongeza mambo fulani ili kiweze kuwa imara zaidi.

Katika kuboresha eneo hilo, aliwafanyisha mazoezi maalumu wachezaji wote wa nafasi hiyo wakiwemo Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Pia kocha huyo ameweka wazi kuwa baada ya winga wake chipukizi, Miraji Athuman, kufungua akaunti ya mabao katika kikosi hicho, amepata mbinu ya kumtumia kwa manufaa zaidi.

Miraji aliyesajiliwa kikosini hapo akitoka Lipuli FC, alifunga bao lake la kwanza la Ligi Kuu Tanzania walipocheza na JKT Tanzania akitokea benchi.

Miraji aliingia kuchukua nafasi ya Deo Kanda na kufanikisha Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa Alhamisi iliyopita Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza na DIMBA Jumatano jana, kocha wa zamani wa Miraji anayekinoa kikosi cha Lipuli, Samwel Moja, alisema mchezaji huyo licha ya kucheza winga, ana uwezo wa kukimbia na mpira hata katikati na kwenda kufunga.

Alisema Miraji anatumia zaidi mguu wa kulia, pamoja na kucheza winga zote, lakini kushoto anakuwa mtamu zaidi kwasababu ndiyo mguu anaotumia.

“Kila kocha ana matumizi yake kwa mchezaji, ila Miraji kwa pale Simba, ana uwezo wa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza kwasababu ni kati ya wachezaji ambao ni hazina ya taifa.

“Kitu cha ziada alichonacho ukiacha mbio, ana uwezo wa kuona goli haraka na kukimbia na mpira kwenda kufunga na ndiyo sababu siku ile aliweza kufunga mapema akitokea benchi,” alisema Moja.

Alifafanua kuwa katika msimu uliopita amefunga mabao matano akiwa na Lipuli FC, anaamini msimu huu anaweza kuongeza zaidi akiwa Msimbazi, ila itategemea na kocha wake atakavyomtumia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here