SHARE

EZEKIEL TENDWA NA CLARA ALPHONCE


 

VITA ya kutaka kuwania uongozi ndani ya Klabu ya Yanga, imezidi kunoga baada ya Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete ambaye ni mtoto wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, naye kutajwa kuitaka nafasi ya uenyekiti.

Ridhiwani aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi na Mweka Hazina wa Ujenzi wa Uwanja wa Yanga wa Kaunda na pia Mwenyekiti wa Kamati ya Uendelezaji ya jengo la klabu hiyo lililopo Mtaa wa Mafia, Kariakoo, Dar es Salaam.

Mbali na mbunge huyo, wengine ambao tayari wameshatajwa kuitaka nafasi hiyo ya uenyekiti ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu hiyo, Hussein Nyika, Rais wa zamani wa klabu hiyo, Tarimba Abas aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa kuajiriwa Jonas Tiboroha pamoja na Katibu Mkuu wa sasa, Charles Boniface Mkwasa.

Taarifa zisizo na shaka kutoka ndani ya Yanga zinadai kuwa, Ridhiwani ameshauriwa na vigogo wakubwa ambao ni mashabiki wa kutupwa wa klabu hiyo kwenda kuinusuru timu na matatizo wanayoyapitia kwa sasa.

Habari zaidi kutoka Yanga zinadai kwamba, Ridhiwani amekubali kubeba jukumu hilo la kuwa mwenyekiti na kinachosubiriwa kwa sasa ni tarehe ya uchaguzi ifike ajitose kwenye uchaguzi.

“Ni kweli kwamba Ridhiwani Kikwete amekubali kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti, amepata ushauri kutoka kwa vigogo wakubwa ambao wengine walishawahi kuwa viongozi wa juu serikalini,” alisema kigogo mmoja ndani ya Yanga.

Alisema moja ya mikakati ya Ridhiwani endapo atapata ridhaa ya wanachama kwenye uchaguzi, ni kuifanya Yanga kuwa kampuni na hapo ataweka viongozi wenye weledi mkubwa na kazi yao.

“Moja ya malengo yake ni kuifanya Yanga kuwa kampuni, amedhamiria kuifanya kuwa moja ya klabu tajiri na anaweza kuwaondoa viongozi wote wanaojali matumbo yao na kuingiza kikosi kazi ili timu yetu isiwe inalia njaa kila mara,” alisema kigogo huyo.

Kutwa nzima ya jana, DIMBA Jumatano lilifanya juhudi ya kumtafuta Rhidhiwani ili kuzungumzia suala hilo bila mafanikio, baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mrefu bila mafanikio.

Na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi kabla ya kwenda mtamboni, hakujibu.

Wakati Mbunge huyo akitajwa kuitaka nafasi hiyo ya uenyekiti, DIMBA Jumatano limenasa barua kutoka Shirikisho la Soka nchini (TFF), ikiitaka Yanga kuitisha uchaguzi mkuu haraka iwezekanavyo kwani uongozi uliopo madarakani muda wao umekwisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here