SHARE

NA MWANANGU NGEMBAH

NANI leo asiyekumbuka mafanikio ya mwanasoka na kocha maarufu duniani, Zinedine Zidane!?

Kama ningeamuru watu wanyanyue vidole juu, nadhani nisingepata hata mmoja, labda asiwe timamu kuhusu masuala ya soka.

Sasa basi nguli huyu, licha ya umaarufu wake uwanjani na yote aliyowahi kuyafanya basi alikumbana na changamoto.

Alipotoka ndani ya klabu ya Juventus alikoishi tangu mwaka 1996 hadi 2001 na kununuliwa kwa fetha nyingi na klabu tajiri ya Real Madrid kule Hispania bado alikumbana na midomo ya wanaojua kulaumu.

Ndani ya siku 100 alipokuwa akiwajibika ndani ya klabu hiyo kongwe, wasemaji walisema kwa sauti na maandishi. Magazeti yakaandika, ‘Siku 100 Zidane anaranda tu Real Madrid’.

Lakini wakati ulipotimia dunia ilimheshimu, sembuse Klaus Kindoki?

Kwanini Kidoki?

Siku moja nilikaa na kocha wa Yanga, mwenye ushawishi mkubwa kuliko makocha wote wa Ligi Kuu kwa sasa.

Tukaongea mengi na kunijibu maswali mengi, muda wote nilikuwa najipanga kumuuliza kuhusu kipa wake, Klaus Kindoki, ambaye yeye ndiye aliyefanikiwa kupata saini yake pale Yanga.

Ndiye anayemjua toka utosi hadi kidole cha mguu, nikitaka kujua kuhusu uwezo na sifa iliyomshawishi kumpa nafasi katika kikosi cha Yanga chenye changamoto ya mashabiki.

Zahera akasisitiza tu kwamba, kipa yule ni mzuri na ana kiwango cha juu, alicheza ligi ya DRC yenye timu kama TP Mazembe, As Vita na nyingine kadhaa maarufu Afrika ije kuwa hii ya hapa Bongo?

Hata baada ya majibu hayo, Wanayanga hawakuonyesha kumwamini Kindoki, ikitokea kipa namba moja ameumia Kindoki ‘akitroti’ wanapiga miluzi ya kukatisha tamaa.

Wakati Kindoni huyu akilalamikia bao alilofungwa mtangulizi wake, Ramadhani Kabwili, dhidi ya Yanga, waliomwona wakamcheka wakidhihaki atua ile!

Leo wamembadilisha jina! Sauti za kumzomea pale Uwanja wa Taifa zimebadilika na kuwa za kumshangilia ndani ua Uwanja wa Majaliwa walipocheza na Namungo FC.

Tayari vichwa vyao vimejaa matumaini ya Kindoki huyu si yule, wameshaanza kurusha makombora dhidi ya kipa mwingine aliyeipa kisogo klabu hiyo, Ben Kakolanya.

Kibao kimoja na Wenge Musica 4×4 wanasema Wenge Toujour likolo (Wenge tuko juu).

Ndani ya wimbo huu kuna maneno yanayowakumbusha mashabiki jinsi awali wanamuziki wa kundi hilo akiwemo Adolph Dominguez, JB Mpiana, Werrason, Alain Makaba, Didier Masela, Blaise Bula kuna sehemu inasema, Meme Seperation ezalaki doleur (Tulipolazimika kugawanyika maumivu yalibaki mioyoni mwetu.

Ndio uhalisia ulivyo kwamba kama Zahera asingeimarisha umoja na kusikia yanayopigiwa kelele, umoja wao ungevunjika na leo Kindoki asingekuwepo Yanga.

Leo hii Kindoki anapaswa kuwasamehe tena 7×70 waliomdhihaki tena basi Wenge walimalizia kwa kutumia neno Towololi bango (Tuwazomee hao), lakini yeye asiwazomee ila ajiimarishe ndani ya goli, apangue mashuti ya ziada kuliko yale ya Namungo.

Siku moja wanazengo hawatapata tabu kutofautisha dirisha na mlango.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here