SHARE

NA MWANDISHI WETU


MWANAMUZIKI nguli wa muziki wa dansi nchini, Hussein Jumbe, juzi alijikuta akimwaga machozi ya furaha wakati wa mazoezi ya pamoja na mastaa wenzake wanaounda kikosi cha timu ya Taifa dansi, yaliyofanyika katika Ukumbi wa CCM Mwinjuma Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea mara baada ya wanamuziki wenzake, Kikumbi Mwanza Mpango na Juma Kakere, kuingiza vipande vipya vya mashairi katika wimbo wa Jumbe ‘Siri ya Nini’, ambavyo vilimsisimua na kujikuta akilia kwa furaha.

“Kiki na Kakere wameniliza kwa kweli, sikutegemea kama wangeweza kunishtua kwa kiasi hiki kwa namna walivyoingiza hisia mpya kwenye wimbo huu na kuifanya Remix kunoga, nimelia kwa furaha kwa kweli”.

Alisema walikuwa wakiufanyia mazoezi wimbo huo bila kupangilia kama wangeongeza kitu chochote, lakini kwa namna kombinesheni ya watatu hao ilivyonoga, atalazimika kuingia nao studio kuurekodi upya.

Mastaa hao wa dansi wako kambini wakijifua kujiandaa na mpambano dhidi ya bendi ya Msondo Ngoma, utakaofanyika Septemba 2, mwaka huu, katika Ukumbi wa Travertine, Magomeni, jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here