Home Habari KIPA MGHANA ASAINI, AANZA KUJIFUA

KIPA MGHANA ASAINI, AANZA KUJIFUA

879
0
SHARE

NA SAADA SALIM


KIPA Mghana aliyetua nchini kujiunga na kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, Simba, Daniel Agyei, amemalizana na uongozi huo baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kisha kwenda kujiunga na wenzake kambini Morogoro kwa ajili ya kukitumikia kikosi hicho kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Kipa huyo amesajiliwa ili kutekeleza mapendekezo ya kocha wa Simba, Joseph Omog ambaye alitaka asajiliwe kipa mwingine kumsaidia kipa Mu- Ivory Coast, Vincent Angban.

Agyei aliyekuwa akiichezea Medeama ya Ghana, sasa ataleta ushindani kwa Angban aliyekuwa kipa namba moja wa Simba na mzawa Manyika Peter ambaye sasa atalazimika kuwa namba tatu.

Rais wa klabu ya Simba, Evance Aveva, ndiye aliyemsainisha kipa huyo mkataba wa mwaka mmoja juzi na kudai amefanya hivyo baada ya benchi la ufundi kuridhika naye, huku pia akiwa amekamilisha vipimo.

Kipa huyo aliwasili nchini tangu wiki iliyopita na kufanyiwa vipimo vya afya, lakini kocha Omog alitaka asisaini mkataba kwanza mpaka amuone.

Imeelezwa kwamba kocha Omog alimfanyia majaribio siku ya Jumamosi na Jumatatu na baada ya kuridhika na kiwango chake akaruhusu uongozi uingie naye mkataba.

Agyei sasa anaungana na wachezaji wenzake kwa safari ya Morogoro kuweka kambi ya maandalizi ya ligi inayotarajiwa kuanza Desemba 17 mwaka huu.

Kipa huyo aliyewahi kuidakia timu ya taifa ya Ghana, pia aliwahi kuwa kipa wa Free State Stars FC ya Afrika Kusini.

Kikosi cha Simba kiliondoka jijini Dar es Salaam jana kuelekea mkoani Morogoro ambako kitaweka kambi kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Katika mechi ya kwanza, Simba inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 35, itafungua dimba na Ndanda FC ya Mtwara mzunguko wa pili utakapoanza Desemba 17.

Hata hivyo, uongozi wa klabu hiyo bado haujaweka wazi ni mchezaji gani atakayekatwa kati ya wachezaji saba wa kigeni waliopo kikosini ambao ndio wanaotakiwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here