Home Habari KIPA WA SIMBA DAY AFARIKI

KIPA WA SIMBA DAY AFARIKI

510
0
SHARE

Na Mwandishi Wetu

KIPA wa Rayon Sports, Evariste Mutuyimana, aliyedaka kwenye mechi dhidi ya Simba siku ya Simba Day kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, amefariki dunia.

Mutuyimana alifariki dunia jana kwenye Hospitali ya Kigali nchini Rwanda.

Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) limethibitisha kutokea kwa kifo cha mchezaji huyo, huku likitoa salamu za pole kwa klabu ya Rayon Sports.

Mchezaji huyo alijiunga na klabu hiyo msimu wa mwaka 2016/17 akitokea Sofapaka FC ya Kenya.

Akizungumzia kuhusiana na kifo hicho, kiungo wa Simba Mnyarwanda Haruna Niyonzima, amesema alimfahamu kipa huyo na ameshtushwa mno na habari za kifo chake.

“Nilimfahamu vizuri sana marehemu… asubuhi nilipotumiwa picha yake na kuambiwa amefariki nilishtuka sana.

“Kinachonihuzunisha zaidi ni kwamba, marafiki zangu wote wanakufa nikiwa huku (Tanzania), inasikitisha sana.

“Tulipocheza nao juzi, siku ya Simba Day, wakati wanaondoka aliugua ghafla ikabidi ndege itue madaktari wamtibie kwanza ndipo waondoke, hivyo bado namkumbuka sana,” alisema Niyonzima kwa masikitiko makubwa.

Alizungumza maneno hayo akiwa nje ya uwanja huku akiwashuhudia wenzake wa Simba wakifanya mazoezi, ambapo yeye alishindwa kufanya hivyo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa malaria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here