Home Uncategorized Klabu ziache usajili wa ujanja ujanja

Klabu ziache usajili wa ujanja ujanja

0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

MUDA mrefu sasa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara imekuwa na changamoto kubwa hasa ya ubora wa wachezaji ambao wanashiriki ligi hiyo, ambayo msimu huu ina timu 16.

Lakini bila kuficha, matatizo ziku zote yamekuwa yakianzia kwenye suala la usajili kwa maana jinsi ya kuwapata wachezaji bora ambao watazitumikia timu hizo.

Pamoja na wingi huo wa timu, lakini wachezaji wengi wanaosajiliwa wamekuwa ni wa viwango vya kawaida tofauti na matarajio ya mashabiki na wadau wengi wa soka.

Kimsingi kumekuwa na tatizo la usajili ambao wachezaji husika wamekuwa hawana mchango unaoeleweka kwa timu zao na hiyo imesababisha kuwepo kwa ligi ya upande mmoja.

Tumeona baadhi ya timu kila mwaka zinasajili wachezaji wapya karibu timu nzima na wanapoulizwa kwanini wanasimamia hoja dhaifu kuwa wanajenga timu.

Ujengaji huu wa timu mara kwa mara ndio umekuwa chanzo cha baadhi ya timu kushindwa kufurukuta katika michuano ya kimataifa na nyingine kushindwa kufanya vizuri katika  Ligi Kuu Tanzania Bara kwa miaka mingi.

Hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa timu nyingi lakini hata zile zilizokuwa zimekaa na vikosi imara kwa muda mrefu nao hawajaepuka kwenye janga hili kwa sababu tu wamekuwa ni watu wa kuamini katika kushinda ingawa uwezo ni mdogo kutokana na ubora wa wachezaji kuwa wa kawaida.

Tumeona jinsi Tanzania ilivyofanywa na baadhi ya wachezaji kuwa shamba la bibi ambalo kila mtu anayetaka kusajiliwa anakuja kwetu kuchukua fedha za bure.

Kimsingi hili jambo halikubaliki kwa namna yoyote kwa sababu ndiyo wamekuwa chanzo cha soka letu kudorora. Ingawa kwa msimu uliopita tumeona mabadiliko kidogo hasa kwa wachezaji wa kigeni, lakini wale wa nyumbani bado tuna matatizo makubwa.

Kiini cha matatizo yaliyopo kwenye soka la Tanzania hasa kwa wachezaji wa ndani ni kukosekana kwa umakini katika usajili lakini kuwepo kwa wachezaji ambao hawajaandaliwa.

Baadhi ya wachezaji wamekuwa hawana viwango vya kucheza kwenye ligi hilo limechangia kwa sehemu kubwa kuwepo kwa ligi dhaifu.

Haya ni mambo ambayo kimsingi hayawezi kuachwa yakaenda hivi hivi, ila lazima mamlaka husika hasa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF)  kuchukua maamuzi sahihi kuhakikisha kuwa ligi inakuwa bora.

Yapo baadhi ya mambo yamekuwa yakijitokeza lakini lazima yafanyiwe kazi kwa uharaka na wepesi ili kuwa na uhakika wa kupatikana kwa matokeo bora kama ambavyo wengi wanahitaji iwe.

Timu zetu zinastahili kuachana na usajili wa ujanja ujanja au vijana wa siku hizi wanasema usajili wa kikanjanja ambao hauna tija kwa timu husika.

Huu ndio msingi wa maendeleo na kama klabu zikiamua kujipanga na kusajili vyema tunaweza kuwa na ligi bora ambayo itakuwa inakidhi matakwa ya nchi na ligi yenyewe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here