Home Makala KLOPP ANAPOTENGENEZA ‘DUDU’ KUBWA LIVERPOOL

KLOPP ANAPOTENGENEZA ‘DUDU’ KUBWA LIVERPOOL

8391
0
SHARE

NA ALLY KAMWE        |    


WAKATI mwingine unahitaji kutuliza akili ya ziada ili uweze kupata majibu ambayo hayawezi kuonekana kwa urahisi na macho, lakini kuna muda inabidi utumie robo ya akili uliyonayo kupata majibu hayo.

Naamini hivi sasa kila mmoja atakuwa anaiwaza Liverpool ya msimu ujao jinsi itakavyokuwa, kwanini usifikiri kwa usajili huu wanaoufanya?

Tofauti na timu nyingine za England kama Manchester United, Manchester City, Tottenham na Chelsea, kwa kipindi chote niliamini Liverpool walikuwa na kikosi cha wachezaji 11 tu.

Ndio, timu pekee ya Liverpool ilikuwa inaanza, hawakuwa na benchi la kutisha kabisa, hawakuwa na sura ya mchezaji mwenye kupeleka taswira mpya uwanjani zaidi ya walioanza.

Tuanze taratibu, hivi ni nani alikuwa na uwezo wa kuchukua nafasi ya Mohamed Salah kutokea benchi, japo kutoa nusu ya ubora wa staa huyo wa Liverpool sasa. Hakuna.

Inawezekana Salah ni kiumbe mwingine, vipi kuhusu Sadio Mane na Firmino? Hao ndio waliibeba Liverpool kwenye mabega yao.

Walifunga mabao mengi kadiri walivyoweza ili kuweka ugumu kwa wapinzani wao, hawakuwa na njia nyingine zaidi ya kufumania nyavu ili kuibeba timu hiyo.

Mapema mwaka huu walimuuza Philippe Coutinho kuelekea Barcelona, ilihitaji kufikiri kidogo, kwa sababu Mbrazil huyo alikuwa nyota wa kikosi hicho.

Hadi anaondoka alikuwa amefunga mabao 12 katika michezo 20, huku akitengeneza nafasi lukuki za mabao.

Kwa kiasi fulani ilitengeneza uwiano mzuri ndani ya kikosi hicho kilichopo Merseyside, lakini kwa jicho la tatu kuondoka kwa Coutinho kumeifanya Liverpool kuwa hivi.

Wachezaji wengi walifunguka na kucheza kwa uwezo mkubwa, inawezekana Coutinho alimuweka Jurgen Klopp katika wakati mgumu kwa kushindwa kuwatumia wachezaji wengine sababu ya uwepo wake.

Baada ya Liverpool kufungwa mabao 3-1 na Real Madrid katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, naona Klopp ameamua kuitengeneza timu hiyo.

Tayari wamekamilisha usajili wa Naby Keita na Fabinho, huku wakisubiri kumtangaza Nabil Fekir kutoka Lyon ya Ufaransa.

Hao ni viungo wa tatu wenye uwezo mkubwa, kwa jinsi tulivyoiona Liverpool ikicheza na ujio wao kuna kitu kikubwa kinatengenezwa na Klopp ndani ya timu hiyo.

Tangu kuanza kwa msimu uliopita, kiungo cha Liverpool kilikuwa chini ya Jordan Henderson, Emre Can na James Milner, lakini pia walikuwepo Georginio Wijnaldum na Oxlade Chamberlain.

Hao wote ni viungo wa kawaida sana, Klopp alitumia akili ya ziada ili wafanye kazi anayoihitaji, lakini kubwa zaidi hawakuwa na sumu kwa wapinzani zaidi ya kasi yao ya kutawanya mipira kwa wachezaji wao watatu wa mbele (Mane, Salah, Firmino).

Keita ni kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kukaba na kushambulia (box to box), Fabinho kwa asili ni mchezaji anayecheza nafasi nyingi uwanjani, lakini amekuwa akitumika sehemu ya kiungo mkabaji (defensive).

Fekir ni kiungo mshambuliaji (attacking), huyu ni mwanadamu muhimu katika utatu huo baada ya wengine wote kufanya kazi yao vizuri.

Fekir ana uwezo mkubwa wa kupiga asisti lakini hata kufunga mabao, amefunga mabao 23 msimu uliopita.

Hao ni wachezaji watatu wanaostahili kuanza katika kikosi hicho, huku tukifikiria zaidi uwepo wa Mane, Firmino na Salah, katika idara ya ushambuliaji.

Kama watafanikiwa kufanya kile walichokifanya katika klabu zao basi Klopp atakuwa ametengeneza mdudu mkubwa ambaye itakuwa ngumu kuuliwa kirahisi.

Kwa hakika itawaongezea upana wa kikosi chao na ikiwezekana hata kufanya mzunguko wa wachezaji kwa urahisi bila kuwa na wasiwasi wa kumkosa mchezaji fulani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here