Home Michezo Kimataifa KLOPP AWATANIA MASHABIKI UNITED, ATAJA MBINU YA KUWAUA MAN CITY

KLOPP AWATANIA MASHABIKI UNITED, ATAJA MBINU YA KUWAUA MAN CITY

5425
0
SHARE

MERSEYSIDE, England


KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp, kumbe naye anauweza utani wa jadi bwana!

Mara baada ya kikosi chake kupangiwa mechi ya robo fainali Champions League dhidi ya Man City, Klopp aliulizwa namna gani anavyouona mtanange huo, akianza kwa kuwatania mashabiki wa Man United.

Alipoulizwa swali la namna anavyouona mchezo, Klopp alitoa jibu hilo ambalo ni tofauti na ilivyotarajiwa kwamba angeigusa mechi yake.

Klopp aliiongoza timu yake hiyo kuing’oa FC Porto kwa jumla ya mabao 5-0 katika mchezo wa hatua ya 16 bora.

Alisema, alitegemea kupangiwa timu ngumu katika hatua ya robo fainali, na hakusikitika aliposikia ni Man City ambao atakutana nao katika hatua hiyo.

“Nafikiri ni mechi iliyosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Manchester United,” alisema Klopp huku akitabasamu.

“Sina hofu, ingawa sio kitu kizuri sana kucheza na timu kutoka nchi moja katika hatua hii ya Champions League, lakini ndio imeshatokea, tutacheza nao na tutakuwa na muda mwingi wa kujiandaa,” aliongeza.

Aidha, Mjerumani huyo alifunguka njia atakayotumia kuimaliza Man City katika mitanange miwili watakayokutana kwenye michuano hiyo.

Klopp alisema kuwa, silaha muhimu kwao ni kucheza soka la kasi na iwapo City hawatocheza kama walivyozoeleka msimu huu, haioni nafasi ya Liverpool kusonga mbele.

Kocha huyo alisema kuwa anaamini, Liverpool itakayoshambulia kwa kasi na nguvu ndiyo itakayoiangusha Man City, timu ambayo inatabiriwa kunyakua taji la Champions League msimu huu.

“Navutiwa na mechi za aina hii. Man City ni timu nzuri na inaeleweka, ukicheza dhidi yao inabidi ufanye kama wanavyofanya wao tena kwa kiwango cha hali ya juu. Huwa hawakabi kulinda matokeo, bali hushambulia kupata mabao mengi zaidi. Inavutia. Na mchezo wa kwanza utakuwa mzuri zaidi,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here