SHARE

MERSEYSIDE, England

NI wivu tu. Unaweza kusema hivyo baada ya kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, kusema anatamani usajili wa Bruno Fernandes kuelekea kwa wapinzani wao Manchester United usifanikiwe.

Ikumbukwe kuwa Manchester United ni wapinzani wa Liverpool, hivyo, ni rahisi kwa wakongwe hao nchini England kuombeana mabaya.

Liverpool walikutana na Sporting Lisbon katika mchezo wa kujiandaa na msimu, huku timu hizo zikitoshana nguvu kwa sare ya mabao 2-2, itakumbukwa kiungo huyo raia wa Ureno alifunga bao moja na kutengeneza lingine.

Baada ya mechi ile, kiwango chake kilimpagawisha Klopp ambaye alisema waziwazi kuwa angekuwa na uwezo angezuia usajili wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25 kwenda Manchester United.

Kocha huyo raia wa Ujerumani alidai kuwa wapinzani wao wana wachezaji wazuri ambao ukiwaongezea wengine wenye ubora kama wao, watakuwa hatari zaidi.

Hivi karibuni baada ya tetesi za Bruno kukaribia kujiunga na Manchester United ziliposambaa, Klopp aliulizwa lakini hakuwa na jibu lingine zaidi ya kuona usajili huo haufanikiwi.

“Bruno Fernandes kwenda Old Trafford? Kama ni hivyo maana yake tutakutana naye ndani ya Ligi Kuu England, kusema kweli ni mchezaji mzuri.

“Tayari ndani ya kikosi chao wana wachezaji wazuri, atawafanya kuwa na nguvu kama akienda pale, ni kitu ambacho sitaki kitokee kwa sasa.

“Si jambo zuri kwetu na wapinzani wengine England au Ulaya, Fernandes ni mmoja wa kiungo bora, alituonyesha kwanini timu kubwa zinahitaji saini yake,” alisema Klopp.

Kumekuwa na tetesi za kiungo huyo aliyefunga mabao 32 msimu uliopita kujiunga na Manchester United ambao wanatajwa kuweka mezani kiasi cha pauni milioni 65 kwa ajili ya fundi huyo wa Kireno.

Hivi karibuni alikaririwa akisema anapenda kucheza nchini England, sababu ni sehemu ambayo soka lao linamvutia.

“Napenda kwenda England, soka lao la kasi na nguvu nalipenda, kwa sasa siwezi kusema chochote bado nipo Sporting Lisbon,” alisema Bruno.

Hata hivyo, kumekuwa na tetesi nyingi zikiwahusisha Manchester Uniteda kuhitaji saini nyingine za akina Christian Eriksen, Ivan Rakitic, Sergej Milinkovic-Savic, and Sean Longstaff. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here