Home Makala KLUIVERT fundi wa mabao ya vichwa kama Mziba

KLUIVERT fundi wa mabao ya vichwa kama Mziba

428
0
SHARE
Patrick Kluivert

NA HENRY PAUL,

UNAPOZUNGUMZIA washambuliaji wataalamu wanaokumbukwa katika historia ya upachika mabao kwa kutumia kichwa, raia wa Uholanzi, Patrick Kluivert, ni miongoni mwa watu waliokuwa na uwezo huo.

Kluivert wakati wa enzi zake za kucheza soka ya ushindani amezichezea klabu kadhaa maarufu duniani kama Barcelona ya Hispania, AC Milan ya Italia, Newcastle United ya England na Ajax ya Uholanzi.

Nyota huyo urefu wa kimo chake wa futi sita na inchi mbili, ndiyo kwa kiasi kikubwa ulimwezesha kupachika mabao kwa kutumia kichwa.

Nyota huyu aligundua faida ya urefu wake, ndiyo maana ilimsaidia kwa sehemu kubwa kuwa na uwezo wa mabao hayo.

Licha ya nyota huyu kuwa mahiri katika kufunga mabao kwa kutumia kichwa, pia alikuwa miongoni mwa washambuliaji waliokuwa na uwezo wa kufunga kwa miguu.

Ubora wa upachikaji mabao wa nyota huyu ulionekana hasa alipokuwa na klabu ya  Barcelona, kwani kwa kipindi cha miaka saba katika timu hiyo, kuanzia 1998 hadi 2004, alicheza michezo 182 na kupachika mabao 90, lakini nusu ya mabao hayo yakiwa ni ya vichwa.

Hivyo hivyo Kluivert akiwa bado na umri mdogo wa miaka 18 mwaka 1995 akichezea klabu Ajax ya Uholanzi aliiwezesha timu hiyo kutwaa taji la UEFA baada ya kuifungia timu yake hiyo bao pekee dhidi ya AC Milan ya Italia.

Nyota huyo alikaa na klabu hiyo kipindi cha miaka minne kuanzia 1994 hadi 1997, ambapo katika kipindi hicho alifanikiwa kuifungia timu hiyo mabao 39 katika mechi 70 alizoichezea.

Kluivert pamoja na kuzichezea kwa mafanikio timu hizo, pia ameichezea timu ya Taifa ya Uholanzi miaka 10 kuanzia 1994 hadi 2004, ambapo katika kipindi hicho aliweza kuifungia mabao 40, ambayo miongoni mwa hayo aliyafunga kwa kutumia kichwa kati ya mechi 79 alizocheza.

Nyota huyo alikuwa ni mchezaji anayeongoza kwa kuifungia timu ya Taifa ya Uholanzi mabao mengi hadi mwaka 2013 alipozidiwa na mshambuliaji Robin Van Persie, ambaye hadi hivi sasa anaongoza kwa kufunga mabao 50.

Umahiri wa upachikaji mabao kwa vichwa nyota huyu, Patrick Kluivert kwa kiasi kikubwa unaweza ukaufananisha na mshambuliaji wa zamani wa Tanzania, Abeid Mziba, maarufu ‘Tekero’, ambaye alitamba akiwa na klabu ya Yanga, Reli za Morogoro, Dodoma na timu ya taifa, Taifa Stars.

Mziba alikuwa miongoni mwa washambuliaji waliotamba katika soka la Tanzania kuanzia miaka ya 1980 hadi 1990 mwanzoni.

Nyota aliyewika  akiwa na klabu ya Yanga, Mziba alikuwa fundi kwa kufunga mabao ya vichwa yaliyomfanya abatizwe jina la Tekero, akifananishwa na mganga maarufu wa tiba za kijadi zamani.

Mshambuliaji huyu wakati anacheza soka alitumia vizuri urefu wa wastani aliokuwa nao kuruka juu na kufunga mabao ya vichwa mithili ya mtu anayepiga shuti kwa mguu na kuwafanya makipa wengi wa timu pinzani kupata wakati mgumu kudaka mipira inayokuwa inaelekea langoni mwao.

Nyota huyo wakati wa enzi zake za kucheza soka ilikuwa ni nadra mno kutoka uwanjani bila kupachika bao na mara nyingi alikuwa akifunga bao moja moja tena kwa kichwa na ndiyo maana wapenzi wa soka nchini wakambatiza jina hilo la Tekero.

Mziba kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 aliyocheza soka ya ushindani kuanzia 1975 hadi 1992 amefunga mabao mengi kwa kutumia kichwa kulinganisha na yale aliyofunga kwa mguu.

Miongoni mwa mabao muhimu aliyofunga kwa kutumia kichwa ilikuwa ni mwaka 1983, wakati Yanga ilipocheza na Reli ya Morogoro maarufu ‘Kiboko cha Vigogo’.

Mziba alifunga bao pekee la ushindi dakika ya 77 akiunganisha kwa kichwa kona ya beki Yusuf Bana (marehemu), ambapo wakati huo Reli ilikuwa ni moto wa kuotea mbali.

Mechi nyingine ilikuwa ni mwaka 1989 katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu), Yanga ilicheza na Ushirika ya Moshi, Mziba aliifungia timu yake ya Yanga bao pekee la ushindi katika dakika ya 75, akiunganisha kwa kichwa krosi ya beki Kenneth Mkapa.

Hivyo utaona kuwa nyota huyu alikuwa ni moto wa kuotea mbali kwa kupachika mabao kwa kutumia kichwa, sawa kabisa na nyota wa zamani wa Uholanzi, Patrick Kluivert, ambaye aliwahi kucheza Barcelona, AC Milan, Ajax, Newcastle United na Valencia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here