Home Burudani KOCHA MPYA YANGA AANZA KAZI RASMI

KOCHA MPYA YANGA AANZA KAZI RASMI

8275
0
SHARE

EZEKIEL TENDWA NA CLARA ALPHONCE


 

YANGA wameangalia namna walivyopata matokeo mabaya katika michezo saba mfululizo, wakagundua kuwa wamewaudhi sana mashabiki wao na sasa wameapa kuwafanyia kitu mbaya Rayon Sports ya Rwanda.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watakutana na Rayon Sports katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo Jumatano.

Yanga wataingia katika mchezo huo huku wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 4-0 na USM Alger ya Algeria hivi karibuni, wakiwa ugenini na kusababisha kuburuza mkia kwenye kundi lao la D, ambalo mbali na Rayon na USM Alger, ipo pia Gor Mahia ya Kenya.

Taarifa njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba, kocha wao mkuu, Zahera Mwinyi, amesema alishazinasa mbinu za wapinzani wao hao na kuzifanyia kazi hivyo kilichobakia ni utekelezaji tu.

Kocha huyo raia wa Congo (DRC), hakuwa kwenye benchi katika baadhi ya michezo, lakini leo anatarajiwa kuongoza vijana wake dhidi ya Rayon.

Uongozi wa Yanga juzi na jana ulikuwa unashughulikia kibali cha kocha huyo ambaye anakabidhiwa mikoba ya George Lwandamina, aliyeamua kutimkia kwao nchini Zambia kujiunga na kikosi chake cha zamani cha Zesco United.

Kocha huyo alisema amewafuatilia wapinzani wao hao na kugundua kuwa ni moja ya timu ngumu lakini watahakikisha wanapambana ili kushinda.

“Wapinzani wetu wazuri hivyo lazima tuingie kwa tahadhari zote, tumewafuatilia na tumeona uzuri na udhaifu wao, hivyo kilichobakia ni kupambana ndani ya uwanja kuhakikisha tunashinda,” alisema.

Tangu kuondoka kwa kocha wao wa zamani, George Lwandamina, Yanga wamecheza michezo saba bila kupata ushindi na leo wamesema iwe jua au mvua kitaeleweka.

Wakati Yanga wakipata matokeo hayo mabaya katika michezo saba, hali ipo kama hiyo kwa Rayon Sport kwani nao wameshindwa kupata matokeo mazuri katika michezo mitano ya hivi karibuni ya Ligi Kuu nchini Rwanda.

Kikosi hicho cha Rayon kinajivunia wachezaji wake wawili ambao wanaijua vizuri Yanga, kwani walishacheza Ligi Kuu Tanzania Bara ambao ni Pierre Kwizera   aliyekuwa Simba na Ismailla Diarra, aliyeichezea Azam FC.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here