SHARE

NA JESSCA NANGAWE

HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba kocha wao mpya, Luc Eymael, raia wa Ubelgiji, tayari ameanza kumwaga madini ndani ya kikosi chake hicho kinachoajiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar.

Eymael ametua Yanga kuchukua mikoba ya Mwinyi Zahera aliyeondolewa kikosini hapo kwa kile kilichodaiwa ni kutokuwa na matokeo ya kuridhisha.

Baada ya kutimka kwa kocha huyo raia wa DRC, kikosi cha Yanga kilikuwa chini ya kocha maarufu katika klabu hiyo, Charles Boniface Mkwassa, na sasa mikoba imerejeshwa kwa Eymael.

Yanga sasa imerejesha akili yake kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuondolewa na Mtibwa Sugar hatua ya nusu fainali kwa mikwaju ya penalty 4-2 visiwani Zanzibar michuano ya Kombe la Mapinduzi na Mbelgiji huyo ameanza kumwaga mbinu zake za kisasa.

Ofisa Mhamasishaji wa klabu hiyo, Antonio Nugaz, ameliambia DIMBA kuwa baada ya vijana hao kumaliza kazi Visiwani Zanzibar, leo wataingia kambini na kesho wataanza rasmi ratiba ya mazoezi chini ya kocha mpya.

“Wachezaji wote wataingia kambini kesho Jumapili (leo), na Jumatatu watakuwa wakifanya mazoezi chini ya kocha wetu mpya, mwalimu amepanga kuwapa mazoezi mara mbili kwa siku kabla ya kucheza na Kagera Sugar siku ya Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam,” alisema.

Aidha kocha huyo anatazamiwa kuja na staili ya aina yake kutokana na taaluma yake ya ukocha ambayo mashabiki wengi wa Jangwani wana shauku ya kutaka kumuona baada ya kusikia alipitia timu kubwa ikiwamo AS Vita ya DR Congo pamoja na Al Merreikh ya Sudan.

Mara baada ya kutua nchini, Eymael alisema anaona fahari kujiunga na moja ya timu kubwa Afrika na anatarajia kuwapa mafanikio makubwa hivyo mashabiki wa Yanga wakae mkao wa kupata furaha.

“Ni furaha yangu kuona kwamba nimepata timu kubwa ndani ya Afrika. Ninaitambua vema falsafa yake na namna ilivyo, hivyo nina imani tutakwenda nayo sawa,” alisema kocha huyo.

Kocha huyo alipomalizana na Yanga alipelekwa Zanzibar kushuhudia kikosi hicho kikicheza michuano ya Mapinduzi na kufungwa na Mtibwa Sugar mabao 4-2 kwa mikwaju ya penalti.

Mbelgiji huyo anatarajiwa kukipika upya kikosi hicho ili kionyeshe kandanda la kuvutia ikizingatiwa kuwa wapo wachezaji mahiri kama Haruna Niyonzima, Feisal Salum, Balama Mapinduzi, Abdulaziz Makame na wengine wapya waliosajiliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here