SHARE

 

George-LwandaminaNA EZEKIEL TENDWA

BAADA ya kuenea tetesi za Yanga kumtaka kocha wa timu ya Zesco ya Zambia, George Lwandamina, ambaye ana historia nzuri ya kutoa vipigo hasa kwa timu za Waarabu, hatimaye kocha huyo ameamua kuanika wazi kila kitu.

Taarifa kutoka Yanga zinadai kuwa uongozi wa klabu hiyo una mpango wa kumleta kocha huyo ili kuchukua nafasi ya Hans Van de Pluijm, ambaye Wanajangwani hao wanafikiria kumpa majukumu mengine ya kuwa Mkurugenzi wa benchi la ufundi.

Taarifa hizo za Lwandamina kuja zinatokana na ukweli kwamba, baadhi ya vigogo wa Yanga wamefuatilia uwezo wake na kuridhika nao hivyo wanataka aje ili kusukuma gurudumu la maendeleo katika klabu hiyo kongwe hapa nchini.

Baada ya taarifa hizo kuenea, DIMBA liliamua kufanya kila linalowezekana kupata mawasiliano ya moja kwa moja na kocha huyo kutoka Zambia ili kuwapa wasomaji ukweli wa mambo.

Kwa bahati nzuri DIMBA likafanikiwa kumpata na kuzungumza naye kwa dakika za kutosha ambapo kwa kinywa chake mwenyewe alikiri kupata ofa kutoka kwa Yanga.

“Nikuambie ukweli rafiki yangu, ni kwamba kuna timu kutoka katika mataifa mbalimbali nimefanya nazo mazungumzo kwa lengo la kuzifundisha. Nikiri kwamba hata hapo Tanzania hiyo timu uliyoitaja (Yanga) wamenifuata,” alisema.

Alisema mbali na Yanga timu nyingine ambayo imemfuata ni Free State kutoka nchini Afrika Kusini, ambayo alikuwa akiichezea winga wa zamani wa Yanga, Azam FC pamoja na Simba, Mrisho Ngassa.

“Ipo pia Free State kutoka nchini Afrika Kusini nao wamenifuata na pia hata timu yangu niliyopo kwa sasa (Zesco) bado wana nia ya kunibakisha kutokana na kazi nzuri ambayo nimewafanyia,” alisema.

Alisema mkataba wake na Zesco unamalizika Februari mwakani hivyo timu ambayo itatoa ofa nono kati ya hizo zinazomhitaji ikiwamo Yanga, hatakuwa na kipingamizi chochote.

“Mkataba wangu na Zesco unamalizika Februari, hivyo timu ambayo itaweka mezani ofa nzuri kati ya hizo ambazo zinanitaka, sitakuwa na kipingamizi chochote.

“Mimi ni kocha na kazi yangu ni kufundisha hivyo siwezi kukataa ninapopata ofa nono, naamini mwisho wa yote itajulikana kwamba nitafundisha timu gani, kwa sasa ngoja nisizungumze mengi,” alisema.

Licha ya kwamba timu kama Free State ya Afrika Kusini wanamtaka lakini huenda kocha huyo akatua Yanga kwani kwa sasa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara fedha kwao si tatizo, wanaweza wakazimwaga ilimradi wanajua nini wanakitaka na kitawaletea nini mbele ya safari yao.

Kama Yanga watafanikiwa kumnasa kocha huyo watakuwa wamelamba dume kutokana na historia yake ya ufundishaji ambayo ilimfanya kutwaa tuzo ya kocha bora wa Zambia mara mbili mfululizo mwaka 2014 na 2015.

Na kazi yake ya kwanza ambayo atatakiwa kuifanya ni kuifikisha Yanga mbali katika michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo ambalo linaweza kuwa dogo kwa kocha huyo kutokana na uzoefu wake.

Lwandamina anajivunia kuiongoza Zesco, kucheza hatua ya Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu ikivuka kwenye kundi A, lililokuwa na timu ngumu kama Al Ahly ya Misri, Wydad Casablanca ya Morocco, na Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Katika kundi hilo walimaliza wakiwa na pointi tisa na kushika nafasi ya pili nyuma ya timu ya Wydad Casablanca ya Morocco, wakizipiga kumbo Al Ahly ambayo mara kadhaa imekuwa ikiisumbua Yanga.

Mbali na Zesco, kocha huyo ameifundisha kwa mafanikio timu ya taifa hilo ambapo mwaka 2005 aliteuliwa kuwa kocha msaidizi chini ya Kalusha Bwalya, akichukua nafasi ya kocha wa zamani wa Simba, Patrick Phiri.

Kocha huyo alipewa jukumu la kuiongoza timu ya taifa ya Zambia kama kocha mkuu Mei 2015, siku tano kabla ya pambano la kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Guinea-Bissau.

Lwandamina aliiongoza timu ya Taifa ya Zambia, kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2016 ambapo walitolewa kwenye hatua ya mtoano na Guinea, kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here