Home Michezo Kimataifa WAMEACHA WALIKOZALIWA, WATAKUWA NA MATAIFA MENGINE URUSI

WAMEACHA WALIKOZALIWA, WATAKUWA NA MATAIFA MENGINE URUSI

8392
0
SHARE

LONDON, England       |   


KWA mashabiki wa kandanda ulimwenguni, kwa sasa hakuna unachoweza kuwaambia kama si kinachohusu fainali za Kombe la Dunia.

Ni vita ya makocha 32, wachezaji 736 itakayozihusisha zaidi ya mechi 300 zitakazoamua bingwa wa michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za timu za taifa.

Hata hivyo, kwa miaka mingi fainali hizo zimekuwa zikiwahusisha wachezaji wanaoyawakilisha mataifa ambayo si walikozaliwa. Safari hii iko hivyo pia na orodha hiyo inawajumuisha mastaa wafuatao.

Hakim Ziyech

Huyu alizaliwa Uholanzi na alicheza ngazi ya timu za vijana. Kutokana na kiwango chake kizuri akiwa na FC Twente, mwaka 2015 aliitwa katika kikosi cha wakubwa kilichokuwa kikinolewa na Guus Hiddink.

Hata hivyo, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25 anayeichezea Ajax, alikataa na miezi michache baadaye alijiunga na Morocco.

Ziyech ambaye ni mkali wa mipira ya faulo, ameshaiwakilisha Morocco katika michezo 15, huku akiifungia mabao nane.

Medhi Benatia

Huyo ni nahodha wa Morocco lakini alizaliwa jijini Marseille, Ufaransa. Alicheza hata U-18 ya Ufaransa mwaka 2005 lakini baadaye aliibukia U-20 ya Morocco.

Mechi yake ya kwanza akiwa na Morocco ni ile ya mwaka 2008 dhidi ya Zambia.

Nyota huyo wa Juventus ameshaiwakilisha Morocco katika mechi 53 na anatarajiwa kuwa mmoja kati ya wachezaji muhimu kwa timu hiyo nchini Urusi.

Kalidou Koulibaly

Alizaliwa Ufaransa na akacheza U-20 ya Ufaransa, lakini Koulibaly aliamua kwenda kuiwakilisha Senegal, uamuzi alioufanya mwaka 2015.

Alifanya hivyo kufuata taifa la wazazi wake japo kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps, alipambana kumshawishi.

Tangu kipindi hicho, Koulibaly ameshatinga ‘uzi’ wa Senegal mara 22 na atakuwa na kikosi hicho katika fainali za nchini Urusi.

Samuel Umtiti

Umtiti alizaliwa Cameroon na hadi akiwa na umri wa miaka miwili, bado alikuwa barani Afrika. Alipokwenda Ufaransa, alichezea timu zote za vijana.

Cameroon walijaribu kumrejesha kwa kumtumia Roger Milla aliyekwenda Ufaransa kumshawishi, lakini alichomoa na mwaka juzi akaitwa kikosi cha wakubwa kilichokwenda Euro.

Aliweza pia kucheza mechi ya robo fainali dhidi ya Iceland ambayo Wafaransa walishinda mabao 5-2.

Raheem Sterling

Ni mzaliwa wa Kingston, Jamaica, lakini atakuwa na kikosi cha England kule Urusi. Sterling alikuwa Jamaica hadi akiwa na umri wa miaka mitano.

Alipoondoka nchini humo, akasajiliwa na ‘academy’ ya QPR kabla ya kwenda Liverpool.

Huko aliweza kuzichezea timu za vijana za England, kabla ya kuitwa katika kikosi cha wakubwa mwaka 2012.

Sterling ameshacheza mechi 38 akiwa na England lakini amefunga mabao mawili pekee. Atakuwa Urusi, sambamba na Harry Kane.

Ivan Rakitic

Atakuwa sehemu ya safu ya kiungo ya Croatia itakayokuwa na Luka Modric, Mateo Kovacic, Milan Badelj na Marcelo Brozovic.

Hata hivyo, licha ya kwamba wazazi wake ni raia wa Croatia, alizaliwa Uswisi na aliiwakilisha katika timu ya U-21. Kuelekea fainali za mwaka huu, ameshaichezea Croatia mechi 91, akifunga mabao 14.

Pepe

Aliondoka kwao Brazil kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 na kwenda Ureno kujiunga na klabu ya Maritimo.

Baba yake aliwahi kusema mwanawe huyo aliitwa na aliyekuwa kocha wa Brazil mwaka 2006, Dunga, lakini alikataa.

Pepe alikuwa na kikosi cha Ureno wakati timu hiyo ikichukua ubingwa wa michuano ya Euro na alikuwa nyota wa mchezo siku ya fainali yao dhidi ya wenyeji Ufaransa.

Akiwa na umri wa miaka 35, Pepe ameshaiwakilisha Ureno katika mechi 91 na safari hii atakuwa nayo Urusi.

Gonzalo Higuain

Wakati anazaliwa, baba yake alikuwa mchezaji wa klabu ya Stade Brestois ya Ufaransa. Hata hivyo, Higuain akahamia Argentina akiwa na umri wa miaka 10 alikojiunga na academy ya River Plate.

Mwaka 2006 akiichezea River Plate, aliyekuwa kocha wa Ufaransa, Raymond Domenech, alimwita kikosini lakini Higuain akakataa, akiichagua Argentina.

Katika mechi zake 70, ameshaipa Argentina mabao 31 akiwa mchezaji wa sita kwa kuwa na mabao mengi katika historia ya timu ya Taifa ya Argentina.

Diego Costa

Costa naye anaingia katika orodha hii ya wanasoka watakaokuwa Urusi na mataifa mengine na si walikozaliwa.

Mwaka 2013, Costa alichezea mechi mbili za kirafiki akiwa na Brazil. Kilichomkimbiza huko ni uwepo wa Fred na Jo ambao walipewa nafasi kubwa mbele ya Costa.

Hata hivyo, kitendo cha nyota huyo kwenda Hispania hakikumpendeza aliyekuwa kocha wa Brazil kipindi hicho, Luiz Felipe Scolari.

Mchezaji huyo alijitetea kuwa haikuwa rahisi kuiacha Brazil alikozaliwa lakini ilikuwa ngumu kuiacha Hispania ambayo ilimthamini kwa kumpa nafasi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here