Home Habari Kumbe dokta wa Terry ndiye mganga wa Walcot

Kumbe dokta wa Terry ndiye mganga wa Walcot

560
0
SHARE

LONDON, England

THEO Walcot ni mtu wa kuchunga sana pindi unapovaana na kikosi cha Arsenal kipindi hiki, yuko kwenye kiwango cha juu sana.

Mpaka sasa amepachika bao 5 kwenye mechi 8 alizocheza, na kama angekuwa na umakini zaidi kwenye pambano dhidi ya Swansea angeweza kufunga mabao mengi zaidi.

Lakini unajua siri ya mafanikio ya Walcott? Unajua kilichobadilika kutoka Theo yule wa Agosti, 2006 alipocheza pambano lake la kwanza pale Emirates, na huyu wa leo? Hapa kuna majibu ya swali hili.

Kabla ya kuanza kwa msimu, Walcott alifanya kikao na jopo la wataalamu kwa ajili ya kukusanya ushauri wa nini anatakiwa afanye kumsaidia kisoka.

Hapa alishauriwa kumtafuta mtu maalumu wa kumpa mazoezi binafsi mbali na ya klabu, lengo likiwa ni kumuweka fiti zaidi na kumpunguzia majeraha ya kila wakati.

Ushauri huu ukamfanya ampe kazi Bradley Simmonds, aliyewahi kuwa mkufunzi binafsi wa mazoezi wa nahodha wa Chelsea, John Terry.

Simmonds amekuwa msaada mkubwa sana kwa wanamichezo na wanamitindo kwa kuweka sawa viungo vyao na kuwafanya kuwa fiti muda wote.

Na kwa muda mfupi aliokaa na Walcot tayari matunda yameanza kuonekana, kwani Theo amekuwa imara na kasi yake imeimarika maradufu.

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, aliweka wazi kuwa Walcott angeweza kufunga hata bao tano dhidi ya Swansea na anaamini kijana wake huyo atakuwa na msimu bora na kuwa chachu ya mafanikio ya Arsenal msimu huu.

“Sijali kuhusu mabao mawili aliyofunga, ninachoamini angeweza kufunga mengi zaidi. Ananipa moyo na ananifanya nione kuna mengi makubwa zaidi yanakuja kutoka kwake,” alisema Wenger.

Pia Wenger amemtabiria Walcot kufunga mabao zaidi ya 20 msimu huu kama akiendelea na kasi aliyokuwa nayo hivi sasa.
Jambo la kushangaza zaidi ni tofauti ya kiwango alichokionyesha Walcot akiwa na kikosi cha Arsenal na akiwa na kikosi cha taifa England.

Akiwa na England kwenye michezo ya kufuzu Kombe la Dunia, Walcot amekuwa akicheza chini ya kiwango, tofauti akiwa na Arsenal.

Kwa miaka 10 aliyokaa Arsenal, msimu wake bora zaidi ni 2012-13, alipofunga mabao 21 katika michezo yote aliyocheza, hapa akaleta faraja japo baadhi walishaanza kumkatia tamaa.

Lakini baada ya hapo akaanza kuandamwa na majeraha na baadaye kidogo jina lake likaingizwa katika orodha ya wachezaji walioshindwa kuipa mafanikio Arsenal tangu mwaka 2004 walipotwaa taji la mwisho la EPL.

Licha ya kushuka kiwango, bado mashabiki wa Arsenal waliendelea kushikilia imani yao, akabaki kuwa Walcot mwenye kasi asiyekuwa na malengo.

Msimu uliopita, rekodi yake kwa msimu ilisimama kwa kufunga mabao 9 kwenye michezo 42, kuna aliyeshtusha na hili? Hakuna, ila mshtuko mkubwa ulikuja alipotemwa kwenye kikosi cha England kilichoshiriki Euro 2016.

Lakini baada ya safari hiyo ndefu ya Theo, msimu kuna kitu tofauti kinaonekana kwenye uchezaji wake na sababu kubwa inatajwa kuwa ni Bradley Simmonds.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here