Home Habari KUMBE JEURI YA BOSOU NI ADEBAYOR!

KUMBE JEURI YA BOSOU NI ADEBAYOR!

750
0
SHARE

SAADA SALIM NA JESCA NANGAWE,

HALI bado haijakaa vizuri kati ya beki kisiki wa Yanga, Vincent Bossou na mashabiki wa kikosi hicho, ambao wamekasirishwa na nyota huyo wa Togo huyo kukataa kucheza mchezo dhidi ya Simba, lakini DIMBA Jumatano limegundua mtu anayempa jeuri.

Beki huyo ameendelea kuweka mgomo wa kuichezea timu hiyo kwa madai ya kutolipwa mshahara wake wa miezi minne, ambapo baadhi ya mashabiki wanadai amechangia kikosi chao kufungwa mabao 2-1 na Simba, kwani angekuwapo huenda hayo yote yasingetokea.

Hata hivyo, wakati kila mmoja akiwa anajiuliza nini hatima ya beki huyo, DIMBA Jumatano limegundua kuwa nahodha wa zamani wa timu ya Taifa ya Togo ambaye ni swahiba wake, Emmanuel Adebayor, anahusika kwa namna moja ama nyingine.

Taarifa za uhakika kutoka kwa rafiki wa karibu wa Bossou, ambaye na yeye mwenyewe amezithibitisha, zinadai kuwa, Adebayor anamtafutia timu ya kuchezea huko Ulaya na atakapomaliza mkataba wake na Yanga msimu huu hataongeza mwingine.

“Nadhani hata yeye mwenyewe ameshaweka wazi kuwa akimaliza mkataba wake hataongeza mwingine, hii inatokana na mambo yao ya chini kwa chini na Emmanuel Adebayor ambaye anahangaika kumtafutia timu ya kucheza barani Ulaya,” alisema rafiki huyo.

DIMBA Jumatano lilikwenda mbali na kumtafuta beki huyo ili kuzungumzia sakala hilo, ambapo alikiri kuwa kuna mambo yake na Adebayor yanayoendelea ambayo asingependa kuyaweka wazi kwa sasa.

“Kwa sasa ninapumzika nyumbani, masuala yote ninamuachia Mungu, kuhusu hilo la kaka yangu Adebayor nisingeweza kuzungumza lolote kwa sasa, ila niseme tu kwamba ni mtu ambaye tunazungumza sana na anajua siri zangu,” alisema.

Akizungumzia kwanini amesusa kuichezea Yanga katika mchezo dhidi ya Simba mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema anaidai timu hiyo mshahara wa miezi mitatu na atakapolipwa hakuna shaka kwamba atajumuika na wenzake.

“Kama nilivyosema bado nipo nyumbani tu napumzika, nina madai yangu ya mshahara wa miezi mitatu, ikiwamo Agosti, Desemba pamoja na Januari na wananizungusha tu, kama wakinipa haki yangu nami nitafanya kazi iliyonileta hapa Tanzania,” alisema.

Akizungumzia mkabata wake na timu hiyo, alisema unamalizika msimu huu na kwa hali ilivyo ni vigumu kuongeza mwingine, huku akidai kuwa, utakapokwisha ndipo anaweza kutoa jibu la moja kwa moja.

Katika hatua nyingine, baada ya beki huyo kudai kuwa anaidai klabu mshahara wa miezi mitatu, DIMBA Jumatano lilimtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, ambapo alisema siyo kweli kwamba Muivory Coast huyo anaidai timu mshahara wa miezi mitatu, badala yake ni mwezi huu tu na kwamba wanasikitika  jinsi anavyoichafua timu mitandaoni.

“Kwanza ametumia njia isiyo sahihi kuichafua klabu kwenye mitandao ya kijamii, tumemwita aje kueleza kwanini anazungumza vitu asivyokuwa na ushahidi navyo, alishaandikiwa hundi yake, lakini hatukuweza kumpa mtu mwingine zaidi yake, haidai klabu pesa yoyote zaidi ya mshahara wa mwezi huu ambapo wachezaji wote wanadai pia,” alisema Mkwasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here