Home Habari KUMBE KWASI KALAMBA ‘MZIGO’ WA MAANA SIMBA

KUMBE KWASI KALAMBA ‘MZIGO’ WA MAANA SIMBA

2667
0
SHARE
NA CLARA ALPHONCE

SIMBA wameshaitumia Lipuli FC kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni 25, kwa ajili ya usajili wa Asante Kwasi, huku beki huyo akiweka mfukoni mwake shilingi milioni 10 na akitarajiwa kulipwa mshahara wa dola 2,000 kwa mwezi, ambazo ni takribani shilingi za Kitanzania milioni 4.5.

Taarifa za ndani kutoka Simba zinadai kuwa, Kwasi amechukua shilingi za Kitanzania milioni 10 za usajili huku akitarajiwa kulipwa mshahara wa dola 2,000 kila mwezi.

Kwasi ambaye ni raia wa Ghana, usajili wake ulikuwa na kizungumkuti kikubwa baada ya Simba kudaiwa na Lipuli kumsajili kinyemela hali iliyofanya baadhi ya viongozi wa kikosi hicho cha Lipuli kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Hata hivyo, baadaye Simba kupitia kwa mwenyekiti wake wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope, walisema wameiandikia Lipuli barua ya kumwomba beki huyo wamsajili kitu ambacho kilifanikisha dili hilo.

Baada ya pande hizo mbili kukubaliana, ndipo jana Lipuli ikaridhia beki huyo kuwa ni mali halali ya Wekundu wa Msimbazi.

Lipuli walifanya hivyo baada ya kuandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwathibitishia kwamba Simba wamewafuata na kukamilisha taratibu za usajili wa Kwasi na sasa wameridhia uhamisho huo.

Kwasi anakwenda kuchukua nafasi ya Mzimbabwe, beki wa kati, Method Mwanjali ambaye ameachwa kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe.

Kwa sasa Kwasi anatarajiwa kuonekana katika michezo inayokuja ya Ligi Kuu na michuano mingine mbalimbali akiwa amevaa jezi za rangi nyekundu na nyeupe akitoana jasho na akina Salim Mbonde, Jjuuko Murushid pamoja na Yusuph Mlipili, kugombania namba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here