SHARE

ABDULAH MKEYENGE

TUNAKWENDA mapumzikoni kwa muda. Tutarudi baadaye kidogo. Kama si Agosti ni Septemba. Ligi ya watoto wa Malkia imemalizika kibabe kama ilivyoanza kibabe.

Utamu wa ligi yao unatokana na matukio mbalimbali ya kumsisimua mtazamaji.

Vijana wa Kiafrika Sadio Mane, Mohamed Salah, Pierre Emerrick-Aubameyang, wamefungana mabao. Kila mmoja amefunga mabao 22.

What are league? Utamu wa ligi yao waliutengeneza. Haujaota kwa bahati mbaya kama uyoga.

Muda huu tunaokwenda mapumziko kwa ligi yao kumalizika, tumebaki na ubishani mitaani. Ubishani tulionao umefanya tujione kama ligi bado inachezwa. Kumbe ligi imemalizika.

Waingereza wamekitengeza kitu hiki. Mabosi wa juu wa TFF yao wanafurahia kuiona dunia ikiwazungumzia wao. Hivi sasa hawajali kinachoendelea katika ligi nyingine. Wanachokijali ni uimara wa ligi yao.

Achana na stori za wao kutoa timu nne zitakazocheza fainali za Ulaya msimu huu (Uefa Champions League na Europa), kwao hii sio stori kubwa. Hata kama wangekosa timu ya kuwawakilisha, bado wangekaa maofisini kwao kugonga mvinyo na wangejiita washindi bila kujali nani atakayewashangaa.

Waingereza wameuuza sana mpira wao. Wameuuza dunia nzima. Ligi ya Hispania ilikuwa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kwa wakati mmoja, lakini kimatangazo bado Waingereza waliwapelekesha katika kuvuta matangazo yenye mkwanja mnene, unadhani faida ikoje hivi sasa ambako Messi na Ronaldo wanacheza ligi tofauti? Kivyovyote vile mapato yamekuwa maradufu.

Wakati soka la Uingereza likiwa na sura hiyo, mtoto mmoja wa kimasikini kutoka Afrika aliyetengeneza jina na pesa nyingi katika ligi hiyo ameamua kustaafu soka. Yaya Toure.

Toure anasimama kama kioo cha juhudi huifanya ndoto iwe. Aliondoka kwao kama kifaranga cha kuku akienda Ulaya njiani akijikunyata kwa baridi kali huko, lakini leo ameacha heshima na jina. Juzi alikuwa katika sherehe za timu yake ya Manchester City kushangilia pamoja ubingwa na kumuaga.

Kupitia Toure wakala wake Dimitri Seluk amevuna mkwanja mnene na kupitia Toure na kupitia Selek, Toure amevuna mkwanja. Hapa kila mmoja ni tajiri. Wenzetu wanaishi hivi.

Ni Seluk aliyetoka hadharani kuuambia uuma kuwa mteja wake anastaafu. Kwa miaka 35 ya Toure angeweza kwenda zake China au Marekani akapige dili za mwisho mwisho mpaka kufikia miaka 38, lakini ameachana nazo, hakutaka tena kusafiri umbali mrefu kila mara kwa ajili ya kucheza.

Alipata kusema msanii wa Bongo Fleva nchini Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ kuwa kuzaliwa masikini sio tatizo, bali tatizo ni kufariki masikini.

Toure alizaliwa masikini, lakini ataenda kufariki akiwa tajiri. Ungeweza kusema utajiri wake aliouvuna unaweza kuisha kama wachezaji wengine, lakini Toure anaishi kwa hofu ya Mungu. Si mtu wa anasa sana kama mastaa wengine wa daraja lake. Ana adabu ya maisha nje ya uwanja.

Alivyokuwa bado anacheza muda wa ligi kumalizika alikuwa anarudi kijijini kwao Ivory Coast kutoa misaada na kupiga picha akiwa karibu na familia yake. Ni tofauti na mastaa wengine ambao huzunguka katika fukwe mbalimbali wakifurahia maisha.

Toure ni mwanadamu wa ajabu sana.
Muda huu alioamua kutundika daluga, huwa namhesabu kama mmoja wa viungo mahiri waliowahi kutokea mbele ya mboni zangu katika bara Afrika, kando ya mwamba mwingine wa Ghana Michael Kojo Essien.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here