Home Michezo Kimataifa KWANINI RONALDO AMEAMUA KUZAA NA GEORGINA?

KWANINI RONALDO AMEAMUA KUZAA NA GEORGINA?

1241
0
SHARE

MADRID, Hispania

CRISTIANO Ronaldo. Si kwamba ni mkali tu wa kutupia mabao uwanjani, bali staa huyu wa Real Madrid, ni balaa kwenye kuchagua warembo.

Tangu mwaka 2002 hadi sasa ameshakuwa kwenye mahusiano na warembo 17. Si mtu wa kutulia na mrembo mmoja kwa muda mrefu.

Na hii ndio sababu iliyofanya mpaka leo watoto wake watatu, Cristiano Jr, Mateo na Eva, kutokujulikana alizaa na mwanamke yupi. Zimebaki kuwa tetesi tu kuwa alipandikiza mbegu.

Baada ya kubwagana na Irina Shanky, hivi sasa yuko kwenye mahusiano na mrembo Georgina Rodriguez, ambaye anaonekana kumtuliza kuliko wanawake wote aliowahi kuwa nao kwenye mahusiano.

Tayari Ronaldo amekiri kuwa mrembo Georgina amebeba ujauzito wake, hii ikiwa mara ya kwanza kwa CR7 kumweka wazi mwanamke atakayemzalia mtoto. Kuna nini kimejificha kwa Georgina?

Ni nani huyu Georgina Rodriguez?

Georgina Rodriguez (22), alikulia maeneo ya Jaca, katika mji mdogo ulio Kaskazini Mashariki mwa Taifa la Hispania.

Mrembo huyu kabla ya kubadili gia na kuingia kwenye masuala ya ‘Umodo’ (urembo na mitindo), baada ya kumaliza masomo ya lugha ya Kiingereza, jijini London, alikuwa dansa katika sherehe mbalimbali.

Ukaribu wa Georgina na Ronaldo ulianza kuonekana kwenye vyombo vya habari, Desemba 2016, walipopigwa picha  ya pamoja wakiwa Paris.

Hivi karibuni Ronaldo alikiri kupitia jarida la El Mundo, kuwa mrembo huyo ni mjamzito, akisema: “Nina furaha sana kupata mtoto na Georgina.”

Walikutana vipi?

Kabla ya kuanza mahusiano na Ronaldo,  Georgina alikuwa akifanya kazi kwenye duka la Gucci, lililopo Madrid, mji mkuu wa Hispania.

Inaamika kuwa mrembo huyu alikutana na Cristiano Ronaldo kwenye moja ya maonyesho ya Dolce & Gabbana.

Baada ya kukutana, wawili hawa walianza uchumba wao kwa siri kabla ya kupigwa picha kwa mara ya kwanza wakiwa Paris, Ufaransa.

Georgina Rodriguez ana msaada wowote kwenye maisha ya mpira ya Ronaldo?

Tayari mashabiki wa soka wameshamshuhudia Georgina katika majukwaa ya Santiago Bernabeu, akifuatilia mechi za Real Madrid, ikiwa ni moja ya kuonyesha kumsapoti mchumba wake.

Na kizuri zaidi, Georgina kila anapokwenda Bernabeu, ni lazima awe ameongozana na mtoto wa CR7, Ronaldo Jr. Hili linatajwa kuchangia baba mtu kujituma zaidi kwa ajili ya kuifurahisha familia yake.

Kwanini Ronaldo ameamua kuzaa na Georgina?

Moja katika mambo yanayotajwa kumfurahisha Ronaldo, ni utulivu wa Georgina ambaye si mrembo anayependa maisha ya kuuza sura kila mara kwenye vyombo vya habari.

Lakini inaonekana Ronaldo amekubali kuzaa na mrembo huyo na huenda akatulia naye, kwa sababu Georgina ni mama mzuri katika malezi ya mapacha wa Ronaldo, Eva na Mateo, ambao inadaiwa mchumba wake aliwapata kwa kupandikiza mbegu.

Ronaldo pia ni baba wa Cristiano Ronaldo Jr mwenye miaka 7, hivyo amejikuta ana amani kwa namna mwanawe anavyoelewana na mrembo Georgina.

Sababu hizo ndizo zinatajwa kumvutia Ronaldo hadi kuamua kuzaa na Georgina na si ajabu siku si nyingi tukamsikia akitangaza ndoa.