SHARE

NA NIHZRATH NTANI,

SAHAU kuhusu alichokisema Marco Van Basten miezi michache iliyopita, mchezaji huyo wa zamani wa AC Milan ya Italia ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Ballon D’or alisema:

“Itachukua miaka mingi zaidi kwa klabu za England kuwekwa katika daraja moja na klabu za La Liga kwa mafanikio uwanjani,” akaendelea kusema: “La Liga ni ligi bora duniani.”

Wiki iliyopita, kiungo wa zamani wa Manchester United ambaye pia ni gwiji wa klabu hiyo, Paul Scholes,  amenukuliwa akikiri kuwa ligi kuu ya Hispania ni ligi bora kuliko ile ya England huku akisisitiza kuwa Hispania wamekusanya wachezaji bora zaidi na wenye vipaji ukilinganisha na EPL.

Ubora wa La Liga  inapelekea kuziona klabu za nchi hiyo zikitawala michuano ya Ulaya. Paulo Scholes anasisitiza La Liga ipo mbele zaidi ya Ligi Kuu ya England.

Michuano ya Ulaya imerejea. Ni mashindano haya pekee ndiyo tunaweza kuyatumia kupima ubora wa ligi ya nchi husika hasa katika ubishani kati ya La Liga na EPL ipi ni ligi bora?

Lakini unapotazama mafanikio ya vilabu vya La Liga katika michuano ya Ulaya, unapaswa kutabasamu tu ikiwa wewe ni shabiki wa ligi kuu ya England. Taji la Mabingwa Ulaya limeweka makazi nchini Hispania kwa miaka mitatu sasa huku wakibadilishana wababe wawili wa nchi hiyo.

Mbali na taji la Europa ambalo ni kama mali ya Sevilla kwa miaka mitatu sasa, klabu ambayo pia inatoka Hispania. Mwisho unabakia kunyamaza tu. Ukimya wenye maumivu mengi ya moyo. Msimu wa nne sasa je klabu za Hispania zitaendelea kutamba ligi ya Mabingwa Ulaya?

REAL MADRID

Kati ya wanadamu wenye bahati duniani ni Zinedine Zidane. Ubora na umahiri wake enzi ya soka lake ni kama maajabu katika macho yetu tuliopata bahati kumshuhudia. Ametwaa kila tuzo akiwa mchezaji iwe ngazi ya klabu ama timu ya taifa.

Lakini kwa sasa ni kocha wa Real Madrid, klabu yake ya mwisho kupata kuichezea. Mpaka sasa amewashangaza wengi. Mbali na kutwaa mataji mawili ndani ya miezi sita tu, ameiongoza klabu hiyo kushinda mechi 15 mfululizo katika ligi.

Historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inawanyima nafasi ya kutetea taji lao tangu ilipobadilishwa jina zaidi ya miaka 20 iliyopita, hakuna klabu iliyowahi kutetea taji lake.

Tunaweza kusema soka si historia, historia haichezi katika soka. Pamoja na klabu hii kutofanya usajili wa kutisha, bado inaweza kutetea ubingwa wake. Ni kwa sababu wana Zinedine Zidane, huyu ni silaha muhimu kwa Real Madrid kuweza kutetea taji lake.

Wana wachezaji mahiri na bora kama Galeth Bale aliye katika ubora wake kwa sasa. Wana Cristiano Ronaldo, Sergio Ramos, Marcelo, Pepe, Modric, Casemiro, Toni Kroos, James Rodriguez ,Isco hata Dan Carvajal. Wakiwa katika ubora wao ni ngumu kuwazuia.

Wamepangwa kundi “F” yenye timu za Sporting Lisbon, Legia na Borrusia Dortmund. Kwenye karatasi wanaweza kuwa wamepangwa kundi linaloonekana jepesi. Lakini soka ni mchezo usiotabirika. Pamoja na hayo ni ngumu mno kwa Real Madrid kushindwa kufuzu hatua ya pili.

Leo watajitupa katika dimba la Santiago Bernabeu kuwakaribisha Sporting CP. Ni mechi muhimu kwao kushinda na mechi muhimu zaidi kwa Cristiano Ronaldo. Kwa mara ya kwanza Ronaldo anakutana na timu iliyosababisha kufika hapo alipo.

BARCELONA

Jana usiku walikuwa wenyeji wa Celtic katika dimba la Nou Camp. Msimu uliopita waliishia hatua ya robo fainali baada ya kuondolewa na Atletico Madrid.

Barcelona msimu huu wapo tofauti na msimu uliopita, ni kama msimu huu hawapo imara zaidi kuliko msimu uliopita. Wamempoteza beki wake wa kulia mahiri kabisa, Dan Alves, huku pia wakimpoteza golikipa wake namba moja, Claudio Bravo, aliyeenda Manchester City.

Ni ngumu kutowapa nafasi Barcelona, tunaweza kuwaona hawa Juni 3, mwaka 2017 kule Cardiff kwenye dimba la Millenium. Mahala ambapo fainali itachezwa.

Bado wana wachezaji wa kutisha akiwemo Lionel Messi, Luis Suarez, Neymar, Rakitic, Pique, Iniesta huku wakiwasili Samuel Umtiti, Andre Gomes, Paco Alcacer.

Wamepangwa kundi “C” likijumlisha kilabu zaa Celtic, Borrusia M’gladbach pamoja na Manchester City. Ni kundi linaloweza kuwa gumu pia lakini haitazamiwi kwa Barcelona kushindwa kufuzu kwenda hatua nyingine.

ATLETICO MADRID

Wakati Zinedine Zidane akionekana binadamu mwenye bahati kubwa, Diego Simeone ni kama anaonekana ana mkosi. Fainali zake mbili ndani ya misimu mitatu ziliisha kwa uchungu mwingi na wenye huzuni.

Msimu huu hawajaanza vyema katika  La Liga , katika mechi tatu wametoa sare mbili na kushinda moja. Sare zao mbili ni dhidi ya timu zilizoonekana dhaifu dhidi yao. Hata hivyo, kwa kiwango walichokionesha katika dimba la Balaidos dhidi ya Celta Vigo, watashangaza msimu huu.

Kwa msimu huu inawezekana ndio klabu pekee ya La Liga iliyosajili wachezaji bora zaidi wakifanya hivyo kwa Kevin Gameiro, Nicolas Gaitan, Sime Vraljiko. Ni usajili wenye akili nyingi.

Mungu akinipa uhai Juni 3, mwaka 2017 nitakuwa katika runinga yangu kuwatazama wakicheza fainali nyingine wanaume wababe hawa wa Jiji la Madrid. Kwanini wasiwe hawa wakati wana wanaume wa shoka hasa. Ukiwa na Antoine Griezmann, Koke, Diego Godin,Torres, Gameiro, Gaitan nini kitakachowazuia?

Wamepangwa kundi “D ” wakiwa na PSV, Rostov na Bayern Munich. Kwa Atletico, hili ni kundi linaloonekana jepesi kwao. Ni ngumu mno kwa Atletico kushindwa kufuzu hatua inayofuata. Jana walikuwa ugenini dhidi ya PSV lakini mechi yao kubwa itakuwa dhidi ya Bayern Munich.

SEVILLA

Kikosi kile kilichocheza dhidi ya Liverpool katika fainali ya Europa hakipo tena. Wamewapoteza Kevin Gameiro, Coke, Ever Banega, Fernando Llorente, Grzgovz Krychowiak ambao walikuwa na usiku bora dhidi ya Liverpool.

Bado pia ikawapoteza Ciro Immobile, Yevhen Konoplyanka, Jose Antonio Reyes. Huku kocha aliyeipa mafanikio makubwa Unai Emery akielekea Ufaransa kunako klabu ya PSG.

Kuwasili kwa Jorge Sampaoli ni kama mapinduzi makubwa ndani ya Sevilla.  Tofauti kubwa ya Sampaoli na Diego Simeone labda ni umri tu lakini wanafanana.

Jorge Sampaoli amewasili na kundi la wachezaji wapya na wenye vipaji wakiwemo Franco Vazquez, Ganso, Wissan Ben Yedder, Luciano Vietto, Silvatore siringu, Joaquin Corea na kiungo fundi Pablo Sarabia.

Kama kuna klabu itakayoshangaza wengi msimu huu, basi ni hii ya Sevilla. Walichokifanya ligi ya Europa kinatosha. Siwaoni kama watashiriki uko msimu huu. Kwa sasa si washiriki tu bali washindani wa ligi ya mabingwa Ulaya msimu huu. Sitashangaa nikiwaona Millenium Juni 3, mwaka 2017 kwenye fainali.

Sevilla wapo kundi “H” lenye timu za Juvetus, Lyon na Dinamo Zagreb. Usiku huu watakuwa mjini Turini kuwafuata Juventus. Ni moja ya mechi kali kabisa kuitazama.

Nafasi ya Sevilla kufuzu ni asilimia kubwa. Mpinzani wake mkubwa ni Juventus. Kwa Sevilla kupita kundi hili haitakuwa bahati, ukiondoa Juventus, inayofuata ni Sevilla kwa ubora. Kumbuka Sevilla ni mabingwa wa Europa baada ya kuifunga Liverpool kipigo cha aibu cha goli 4 . Ni Liverpool hii ya Jurgen Klop. Hawana cha kupoteza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here