Home Michezo Kimataifa LEICESTER WAPO WANAPOSTAHILI KUWAPO

LEICESTER WAPO WANAPOSTAHILI KUWAPO

476
0
SHARE

LEICESTER, England

WAKO wanaosema ni uchovu wa msimu uliopita, wako pia wanaosema hii ndio Leicester halisi, kila mtu anasema la kwake, lakini nini hasa kinachosababisha bingwa mtetezi kupoteza dira msimu huu?

Bado linabaki kuwa swali gumu kwa wapenzi wa soka.

Bila shaka hakuna timu iliyokuwa ngumu kufungika msimu wa 2015-16 kama Leicester, kwa kiwango chao, halikuwa jambo la ajabu kuona wakibeba taji la kwanza la Premier League katika historia ya klabu hiyo.

Wakashika kila kona, habari zao zikajadiliwa kila dakika, hakika hata asiyekuwa shabiki wa soka alitamani kujua kidogo kuhusu hadithi yao iliyofanana na kisa cha Mfalme Daudi na Goliati.

Lakini mambo ni tofauti msimu huu, si kwamba hawako kwenye mbio za kutetea taji lao, ukiiutazama msimamo wa Premier League utagundua kuwa Leicester ni miongoni mwa timu zilizo kwenye hatari ya kushuka daraja msimu huu.

Msimu huu wameshinda minne kati ya 18 waliyocheza mpaka sasa kwenye Premier League (sare tano na kufungwa mara 9), hii ni tofauti na msimu uliopita walipopoteza michezo mitatu tu kati ya 38 waliyocheza.

“Hali ngumu sana,” alikaririwa kocha wao Claudio Ranieri mwanzoni mwa Desemba. “Kila kitu kilikuwa sawa msimu uliopita, tulianza kwa bahati na tukamaliza hivyo, msimu huu kila kitu kimebadilika.”

Lakini mbali na ubovu wa Leicester kwenye Premier League msimu huu, wameonekana kuwa tofauti pindi wanapocheza mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo wanatarajiwa kuvaana na Sevilla kwenye hatua ya 16 bora baada ya kumaliza wakiwa vinara wa kundi G.

Msimu huu Leicester wamekuwa dhaifu pia katika uwanja wao wa nyumbani, wakiambulia sare moja tu na kufungwa nane katika mechi 18 walizocheza mpaka sasa.

Safu yao ya ulinzi imekuwa nyanya msimu huu waliruhusu kufungwa mabao 19 katika viwanja vya ugenini mpaka sasa, lakini ikumbukwe msimu uliopita walifungwa mabao 20 tu katika mechi zote walizocheza ugenini.

“Kwenye ligi ya mabingwa tunacheza vyema lakini kwenye ligi tuko ovyo sana, ukiniuliza kwanini, sijui pia,” alisema Ranieri alipohojiwa na mtandao wa ESPN.

Msimu huu Leicester hawako vizuri pia katika eneo la ushambuliaji. Mpaka sasa wamefunga mabao 23 kwenye michezo 18. Msimu uliopita katika idadi ya michezo hii, walifunga mabao 36.

Kasi ya ufungaji wa straika wao Jamie Vardy aliyemaliza nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora msimu uliopita nyuma ya straika wa Tottenham, Harry Kane, imeshuka kama si kupotea kabisa.

Kwenye mechi 18 alizocheza mpaka sasa, Vardy amefunga mabao matano tu, akizidiwa mabao nane na kinara Diego Costa aliyefunga mara 13.

Kiwango cha Riyad Mahrez (25) kimeshuka pia msimu huu. Baada ya kumaliza kwenye nafasi ya tano msimu uliopita kwenye orodha ya wafungaji bora akiwa na mabao 17, msimu huu katika mechi 18 amefunga mabao matatu tu.

Ukijumlisha na hasara ya kumpoteza kiungo N’Golo Kanté aliyesajiliwa na Chelsea msimu huu, bila shaka utaona ni majanga kiasi gani yanayowakabili Leicester msimu huu.

Kweli ligi bado ina safari ndefu hadi kuifikia michezo 38 ya msimu, lakini ukweli usiopingika ni kuwa Leicester wamepotea na wasipokuwa makini, watazidi kupotea zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here