SHARE

MERSEYSIDE, England

WAPO wanaodai eti Liverpool ikiimchapa Manchester City basi ubingwa wa Ligi Kuu England ndio umeenda Anfield.

Lakini ukweli ni kwamba EPL si ligi ya kumalizika ndani ya miezi michache, hutokea lakini ni kwa bahati.

Na pia ratiba ya Liverpool ni ngumu mno. Labda kama kauli ya kusema Liverpool itakuwa bingwa baada ya kuifunga Man City leo inatumika kuteka tu hisia. Hapo wataeleweka.

Hata kama Liverpool itashinda leo, kuna vitu vinaweza kutokea huko mbele ya safari. Mosi, wanaweza kuanza kupoteza pointi muhimu (si lazima iwe kwa kupoteza mechi).

Na pili, utafika wakati Man City itaanza kushinda mechi zake mfululizo, kama ilivyofanya msimu uliopita.

Na safari itakuwa ngumu kupita maelezo kama mmoja wa washambuliaji watatu wa Liverpool akapata jeraha kubwa.

Ushindi ambao Liverpool itaupata leo utaifanya timu hiyo iimarike kisaikolojia. Changanya hilo na imani iliyopo ndani ya klabu kwamba mwaka huu ni wao.

Changanya na namna wanavyoshinda mechi zao hata wanapocheza chini ya kiwango.

Liverpool inatakiwa kucheza soka la kikatili mno leo dhidi ya Man City. Inatakiwa kufanya vile inavyofanya siku zote inapocheza Anfield.

Man City ni wadhaifu mno katika safu ya ulinzi na hali itakuwa mbaya zaidi kama mlinda mlango wake, Ederson, hatacheza leo.

Kipa chaguo la pili, Claudio Bravo, bado hajaizoea EPL. Si mtulivu katika matukio na hilo lilionekana kwa kadi nyekundu aliyoonyeshwa dhidi ya Atalanta wiki hii.

Man City pia ina tatizo kubwa la nani atakayecheza beki wa kati. Kama Fernandinho atatumika hapo, ina maana watakosa ulinzi katika eneo la kiungo.

Kama atacheza Nicolas Otamendi, basi ni lazima atatoa ‘boko’ na ni beki pekee wa City ambaye hachezi kama Guardiola anavyotaka walinzi wake wacheze.

Hivyo, Liverpool italazimika kutumia udhaifu huo kushinda mechi. Hawatakiwi kubutua mipira hovyo. 

Ili Man City ishinde itatakiwa kufunga angalau mabao mawili. Na ina uwezo wa kufanya hivyo.

Kinachotisha hilo kutokea ni kwamba, Sergio Aguero hajafunga au kupata ushindi katika mechi 10 alizocheza Anfield. Huyo ndiye mshambuliaji tegemeo wa Man City.

Kingine ni Raheem Sterling. Huyu ni mmoja wa wachezaji bora duniani hivi sasa, lakini anapowasili Anfield, huingiwa na mchecheto. Mara nyingi hushindwa kuwa msaada kwa Man City na kwa siku ya leo watamhitaji zaidi ya miaka yote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here