Home Michezo Kimataifa LEO TENA

LEO TENA

1570
0
SHARE

*Usiku wa Ulaya kuendelea kwa mechi kali tena

*Barca kulipa kisasi kwa Inter Milan bila Messi, Ancelotti atamba kuichapa PSG

*Reus, Griezmann ni vita ya kuongoza kundi

CATALUNYA, Hispania

MECHI za Ligi ya Mabingwa Ulaya zinendelea tena usiku wa leo baada ya nyingine kutimua vumbi jana katika viwanja mbalimbali barani Ulaya, huku mchezo wa Manchester United dhidi ya Juventus ukiwa kivutio zaidi.

Katika mzunguko wa tatu wa michuano hiyo mikubwa Ulaya, ushindani umekuwa mkubwa zaidi kwa kila timu kuhitaji pointi tatu ili kujihakikisha nafasi ya kusonga kwenye hatua zinazofuata.

Tofauti na ilivyozoeleka, msimu huu michuano hiyo inaonekana imeshika kasi zaidi kwa michezo mikubwa kuchezwa mapema katika hatua ya makundi.

Huku ikikumbukwa kuwa zamani michezo ya aina hiyo ilizikutanisha timu hizo kuanzia katika hatua za mtoano mpaka kufikia ya mwisho, yaani fainali.

Usiku wa leo kuna michezo ambayo itakufanya usahau kulala kabisa, katika Uwanja wa Nou Camp, Barcelona wanaikaribisha Inter Milan huku jijini Paris wakishuhudia mchezo mkali kati ya PSG na Napoli, upande mwingine Borrusia Dortmund watakuwa wenyeji wa Atletico Madrid kwenye Uwanja wa Signal Iduna Park.

BARCELONA v INTER MILAN

Kubwa ambalo linakumbukwa pindi timu hizo zilipokutana mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2010, huku Barcelona ikiwa chini ya Pep Guardiola na Inter Milan ilikuwa ikifundishwa na Jose Mourinho.

Barcelona walishindwa kufua dafu mbele ya kikosi hicho cha Mourinho kilichotamba kuwa na ulinzi mkali na mwisho wa siku Inter Milan ilifanikiwa kutinga hatua ya fainali ambayo waliwafunga Bayern Munich mabao 2-0.

Leo Barcelona itakosa huduma ya Lionel Messi, aliyeumia mkono katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania dhidi ya Sevilla wikiendi iliyopita, katika ushindi wa mabao 4-2.

Messi atakuwa nje kwa wiki tatu ambazo zitamfanya kukosa mchezo wa El Classico dhidi ya Real Madrid.

Upande wa Inter Milan watamkosa kiungo wao, Radja Nainggolan, aliyepata majeraha ya enka katika mchezo dhidi ya AC Milan uliomalizika kwa Mauro Icardi kuifungia bao pekee Inter Milan dakika ya 90.

Pia, Ivan Perisic na Marcelo Brozovic wanaweza kukosa mchezo wa leo baada ya wachezaji hao wote kupata majeraha dhidi ya AC Milan wikiendi iliyopita.

Mchezo mwingine katika Kundi B utazikutanisha timu za PSV na Tottenham, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Phillips Stadion.

PSG v NAPOLI

Moja ya michezo mikali inayopatikana katika kundi gumu kwenye michuano ya msimu huu, kwenye Uwanja wa Parc de Princes, PSG wataikaribisha Napoli kutoka nchini Italia.

Kocha wa Napoli, Carlo Ancelotti, anarejea kwa mara kwanza nchini Ufaransa kucheza dhidi ya timu yake ya zamani, huku akikumbukwa kuwa mmoja wa makocha walioipa mafanikio klabu hiyo tajiri Ufaransa.

Napoli ni vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi nne, wakifuatiwa na Liverpool wenye pointi tatu sawa na PSG, huku timu ya Red Star ikikamata mkia kwa kuwa na pointi moja.

Beki wa PSG, Thiago Silva, hatihati kuukosa mchezo huo, ikitajwa alipata majeraha ya enka katika mchezo uliopita.

Napoli hawana taarifa za majeruhi hata mmoja, wakiingia kamili katika mchezo huo mkali wa kuhitaji pointi tatu zitakazowafanya kuendelea kuongoza Kundi C.

Mchezo mwingine katika kundi hilo utapigwa kwenye Uwanja wa Anfield kati ya Liverpool dhidi ya Red Star.

DORTMUND v ATLETICO MADRID

Timu ya Borrusia Dortmund wapo katika kiwango kizuri sana tangu kuanza kwa msimu huu, wakiwa vinara wa Ligi Kuu Ujerumani baada ya kucheza michezo nane.

Upande wa pili, Atletico Madrid wanasifika kwa soka la nguvu na kasi huku wakiwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kubadili matokeo wakati wowote uwanjani.

Antoine Griezmann, Diego Costa, Koke, Saul Niguez na wengine wengi, huku wenyeji wa mchezo huo wakijivunia uwepo wa Marco Reus, Paco Alcacer, Axel Witsel, Christian Pulisic, Jadon Sancho na wengine wengi.

Mchezo huo wa Kundi A ni mkali kutokana na kila timu kuhitaji pointi tatu za kuongoza kundi hilo, ikiwa wote wana pointi sita baadaya kushinda michezo miwili ya awali dhidi ya Mon aco na Club Brugge.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here