SHARE

MERSEYSIDE, England


KIKOSI cha Kocha Jurgen Klopp, Liverpool, kimezidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England, baada ya jana kuibuka na ushindi wa sita mfululizo msimu huu, kikiinyuka Southampton mabao 3-0.

Mechi hiyo iliyochezwa katika uwanja wa Anfield jana, ilishuhudiwa na zaidi ya mashabiki 50,000 na hawakuangushwa na vijana wao ambao mapema wiki hii waliifunga PSG mabao 3-2 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Klopp alifanya mabadiliko machache katika kikosi chake hicho kilichochuana na PSG, kwa kuwaanzisha Roberto Firmino, Xherdan Shaqiri na Joel Matip, ambao walichukua nafasi za Daniel Sturridge, James Milner na Joe Gomez.

Wenyeji hao katika mchezo huo, Liverpool, ndio walioanza kuonja raha ya mabao baada ya shuti la winga Shaqiri kuguswa na beki wa Southampton, Wesley Hoedt, kabla ya kutinga wavuni katika dakika ya 10.

Bao hilo la kujifunga lilionekana kuwachanganya Southampton, na dakika 11 baadaye walipachikwa bao jingine lililowekwa kimiani na beki Matip, akiunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na Trent-Alexander Arnold.

Katika dakika ya 45 ya mchezo huo, Liverpool walipata ‘frikiki’ ambayo ilipigwa kiufundi na Shaqiri, lakini shuti lake liligonga mwamba kabla ya kumaliziwa na Mohamed Salah.

Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, Liverpool walitoka dimbani kifua mbele kwa uongozi wa mabao 3-0.

Hata hivyo, dakika 45 za kipindi cha pili zilimalizika bila timu hizo kuongeza bao jingine, huku bao la Salah likikataliwa na mwamuzi kwa madai kuwa aliotea kabla ya kutupia mpira kwenye nyavu.

Beki, Virgil van Dijk alishindwa kumaliza mchezo huo kutokana na jeraha la mbavu alilokumbana nalo, ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Gomez.

Mechi nyingine kali ya jana ilikuwa ni kati ya Man United dhidi ya Wolves, ambayo ilichezwa kwenye Uwanja wa Old Trafford na mmoja wa mashabiki waliohudhuria alikuwa ni kocha wao wa zamani, Sir Alex Ferguson.

Ferguson alirejea kwenye dimba hilo na kupokelewa vyema na mashabiki, ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipofanyiwa upasuaji wa dharura katika ubongo wake, Mei mwaka huu.

Lakini, Man United walishindwa kumkaribisha kocha wao huyo wa zamani kwa ushindi, baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na vijana hao wa Wolves.

United waliandika bao la kwanza kupitia kwa Fred, baada ya kupokea pasi ya mwisho ya Paul Pogba na Mbrazil huyo hakufanya makosa, akiukwamisha mpira kwenye nyavu za pembeni kwa shuti maridadi.

Wolves, ambayo imepanda daraja msimu huu, iligoma kukata tamaa na kupambana vilivyo hadi walipoweza kusawazisha bao hilo, lililofungwa na kiungo Joao Moutinho, akimalizia vyema pasi ya mwisho ya straika, Raul Jimenez.

Nao mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Man City, walizimalizia hasira zao kwa Cardiff City kwa kuwapa kichapo kikali cha mabao 5-0, wakiwa ugenini.

City, ambao mapema wiki hii walianza msimu wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kupoteza mbele ya Lyon mabao 2-1, huku wakimkosa kocha wao, Pep Guardiola, aliyekuwa anatumikia adhabu, walirudi na kasi hiyo jana.

Mabao ya Sergio Aguero, Bernado Silva, Ilkay Gundogan na winga, Riyad Mahrez aliyevunja rekodi ya usajili katika kikosi hicho, yalitosha kuifanya City izidi kuwapa presha Liverpool na Chelsea katika vita ya ubingwa msimu huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here