Home Makala LIVERPOOL NI SASA AU TUSUBIRI NYAKATI NYINGINE TENA?

LIVERPOOL NI SASA AU TUSUBIRI NYAKATI NYINGINE TENA?

3337
0
SHARE

NA NIHZRATH NTANI

NIMEKUMBUKA zamani, sanduku la posta ndio ilikuwa sehemu ya pekee ya kuwasiliana na ndugu ama rafiki aliye mbali. Maendeleo ya sayansi na teknolojia hayakuwa kama yalivyo hivi leo.

Noti yenye thamani kubwa kabisa nchini ilikuwa shilingi 1000. Wakati huo hakukuwa na noti ya shilingi 5,000 na 10,000 kama ilivyo hivi leo.

Ukuta ulioitenganisha Ujerumani Magharibi na Ujerumani Mashariki ulikuwa unavunjwa na kuunda Taifa moja la Ujerumani. Kumbukumbu za zamani zinarejea.

Ni kipindi ambacho stendi kuu ya mabasi ya mikoani ilikuwa pale Kisutu. Maeneo ya Kimara hadi Mbezi kote kumezungukwa na msitu.

Ni miaka 28 iliyopita angali bado nina kumbukumbu nyingi dhidi ya nyakati hizo. Nakumbuka mengi ya zamani.

KWANINI NIMEKUMBUKA ZAMANI?

Ni kwa sababu ya historia kuwa na sifa ya kuishi. Historia inazungumza. Ni historia kuhusu klabu ya Liverpool.

Jumamosi ya Aprili 28,1990. Liverpool chini ya Meneja, Kenny Daglish, wanaifunga QPR kwa ushindi wa mabao 2-1 na kutwaa taji la Ligi Daraja la Kwanza ya Uingereza kabla ya kubadilishwa jina miaka miwili baadaye na kuitwa Ligi Kuu ya Uingereza. Macho yetu yangali yanakumbuka mengi.

Kikosi cha Daglish kiliwapa furaha mashabiki wa Liverpool usiku huo. Hilo lilikuwa taji lao la 18 tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo.Wakati Liverpool wakiwa na mataji 18 mkononi. Manchester United walikuwa na mataji 7 tu ya ligi. Miaka 28 baada ya tukio hilo.

Manchester United wamekwishatwaa jumla ya mataji 20 ya Ligi Kuu huku Liverpool wakibakia na mataji yao yale yale. Huzuni iliyoje!

JE, LIVERPOOL INA LAANA?

Katika soka ipo imani kama hii. Mashabiki wengi wa soka wanaamini kuwa ipo laana kunako klabu ya Benfica kuhusu kutwaa taji katika michuano ya Ulaya.

Bado pia kuna imani kuhusu klabu ya Juventus ya Italia. Nayo pia inasemekana ina laana na taji la michuano ya mabingwa barani Ulaya. Ipo imani kumhusu Jurgen Klopp’s. Yeye ni mshindwa wa fainali siku zote. Achana na simulizi za wote hao.

Kwa zaidi ya misimu 15 iliyopita. Klabu inayokuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza mpaka kufikia Sikukuu ya Krismasi ndiye anayekuja kuwa bingwa wa ligi hiyo.

Hata hivyo, hadithi huwa tofauti kwa upande wa Liverpool. Mara mbili walipata kuwa kileleni katika wakati wa Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya. Mwishowe waliishia kulitazama taji hilo likienda kwa wapinzani wao bila kutarajia.

Mashabiki wa Liverpool bado wangali na kumbukumbu ya msimu wa 2008/2009. Chini ya Rafael Benitez, mbio za ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza zilionekana kama zimekwishamalizika kwa Liverpool kupewa nafasi kubwa kutwaa taji hilo, baada ya kuwa kileleni wakati wa sherehe za Krismasi.

Mwisho wa msimu ni Manchester United wakaishia kutwaa taji hilo na kupeleka huzuni ndani ya Jiji la Liverpool.

Matumaini yakarejea tena msimu wa 2013/2014. Chini ya Meneja Brendan Rogers. Liverpool walikuwa katika Sikukuu ya Krimasi. Zilibakia mechi tatu tu kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo. Huku Liverpool wakiwa kileleni kwa tofauti ya alama tano dhidi ya Manchester City.

Ni Manchester City waliokuja kutwaa taji hilo katika hali ya mshangao zaidi. Huku ikiiacha Liverpool katika simanzi kuu.

JE, WANAWEZA KUTWAA TAJI MSIMU HUU?

Wakiwa kileleni kwa tofauti ya alama nne dhidi ya Manchester City, huku wote wakishuka dimbani mara 21. Kihesabu zimebakia mechi 17 kabla ya kuhitimisha ligi hiyo.

Mashabiki wengi wa Liverpool wameanza kujipa matumaini makubwa ya kuona timu yao ikitwaa taji hilo msimu huu. Taji wanalolisubiri kwa miaka 28 hadi sasa.

Kikosi cha Jurgen Klopp’s kinaonekana kuwa ni kikosi bora na kilichokamilika zaidi kuliko vikosi walivyokuwa navyo Rafel Benitez na Brendan Rogers.

Wakati ukijaribu kufungua kumbukumbu dhidi yao, unapaswa ukae kimya. Historia ya Liverpool inasikitisha. Ni kama wenye laana na taji la Ligi Kuu ya Uingereza. Nini kinawasibu Liverpool kwenye mbio hizi?

Bila shaka, tunaweza kuiweka Liverpool kwenye kundi la Benfica, Juventus na kocha Jurgen Klopp’s ikiwa watashindwa kutwaa taji msimu huu. Kikosi hiki kinastahili kuvunja laana hii. Hatuwezi kusubiri nyakati nyingine tena.

@@@@@@@@@@@@@@@@

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here