Home Michezo Kimataifa LOUIS VAN GAAL SOKA KWAKE NDIO BASI TENA

LOUIS VAN GAAL SOKA KWAKE NDIO BASI TENA

343
0
SHARE
Louis van Gaal

LONDON, England

HABARI iliyoteka vichwa vya habari za michezo ulimwenguni kote kwa sasa ni ile ya kocha wa zamani wa Manchester United, Louis van Gaal, kuacahana na kazi hiyo ya kufundisha soka.

Kocha huyo wa zamani wa Ajax na Barcelona, ametangaza rasmi kustaafu soka.

Van Gaal amedai kuwa amefikia uamuzi huo kutokana na sababu mbalimbali za kifamilia.

Mkufunzi huyo raia wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 65, amekuwa nje ya kazi hiyo tangu alipofungashiwa virago pale Man United.

Van Gal alitimuliwa Old Trafford mwishoni mwa msimu uliopita kutokana na mwenendo usioridhisha wa kikosi hicho.

Hata hivyo, si kwamba Mholanzi huyo hakupata ofa kutoka katika klabu mbalimbali, aliamua tu kupumzika.

Kwa mujibu wa gazeti moja la De Telegraaf, Van Gaal, amekataa dili nyingi za kuzinoa klabu za China ikiwamo moja ambayo ilikuwa tayari kumlipa pauni milioni 44 kwa misimu mitatu.

“Ningeweza kwenda pale, lakini kuna mambo ya kifamilia,” alisema Van Gaal.

Hata hivyo, moja ya sababu za kifamilia ambazo zimekuwa zikitajwa kuchochea uamuzi wa Van Gaal kuachana na soka, ni ile inayomhusu mmoja wa binti zake.

Imeelezwa kuwa mrembo huyo alifiwa na mumewe mwezi uliopita na jambo hilo linamuumiza kichwa kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich.

“Nilifikiria kuwa natakiwa kuachana na soka, nilikuwa kwenye wakati mgumu. Lakini sifikirii kurudi kwenye soka,” alisema.

Licha ya kupitia kwenye wakati mgumu kwa kipindi chote alichokaa Old Trafford, Van Gaal aliiwezesha ManĀ  United kuchukua taji la FA.

Michuano hiyo ilikuwa ya mwisho kwa Mholanzi huyo pale Old Trafford ambapo aliifunga Crystal Palace mabao 2-1 katika mtanange wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Wembley.

Lakini pia, hilo lilikuwa taji lake la 20 tangu alipoanza kufundisha soka.

Mpaka anatangaza kustaafu hivi karibuni, Van Gaal, alikuwa ameshashinda mataji saba katika ligi alizofundisha soka, huku akiwa mshindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mke wake alifariki kwa kansa

akiwa na umri wa miaka 18, Van Gaal alikutana na mke wake wa kwanza, Fernanda Obbes.

Walioana na kubahatika kuzaa watoto wawili, Brenda na Renate. Obbes alifariki mwaka 1994 na kilichosababisha umauti wake ni ugonjwa hatari wa kansa.

Mwaka 2008, Van Gaal, alimuoa Truus, mwanamke raia wa Ureno, ambaye anaishi naye hadi hivi sasa.

Van Gaal ni Mkatoliki

Kocha huyo ni mkiristo wa dhehebu la Katoliki. Inaelezwa kuwa hata mke wake wa kwanza, Obbes, alikutana naye katika maombi ya kanisani.

Utajiri wake

Van Gaal ni mmoja kati ya makocha wenye kipato kikubwa barani Ulaya. Kwa sasa anatajwa kuwa na utajiri wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 18 (zaidi ya Sh bilioni 39 za Kitanzania).

Mourinho ni mwanafunzi wa Van Gaal

Wakati Louis van Gaal alipokuwa akiinoa Barcelona miaka mingi iliyopita, Jose Mourinho alikuwa klabuni hapo.

Kipindi hicho Mourinho alikuwa mkalimani wa Mholanzi huyo, kwani alikuwa na uwezo wa kuzungumza lugha.

Astaafu na tuzo mkononi

Jumatatu ya wiki hii, Serikali ya Uholanzi ilimkabidhi tuzo ya heshima Van Gaal kwa mchango wake katika mendeleo ya soka nchini humo.

Mbali na mafanikio mengine, itakumbukwa kuwa Van Gaal aliiwezesha Uholanzi kushika nafasi ya tatu katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 zilizofanyika nchini Brazil.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here